Jul 20, 2017 14:09 UTC
  • Malalamiko ya Wasaudia yamfanya mfalme amchukulie hatua mwanamfalme

Kitendo cha kuenea video inayomuonyesha mwanamfalme mmoja akifanya ukatili dhidi ya raia wa Saudia, kimeibua hasira kali na ukosoaji mkubwa wa Wasaudi katika mitandao mbalimbali ya kijamii hususan Twitter, na hivyo kumfanya Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud kutoa amri ya kutiwa mbaroni mwanamfalme huyo.

Video hiyo iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, inamuonyesha mwanamfalme huyo Bin Abdulaziz Bin Musaid Al Saud, akiwashambulia kwa kuwapiga mateke raia kadhaa wa Saudia wakiwamo wanawake huku akiwaita kwa jina la watumwa.

Wanamfalme wa Saudia

Kufuatia kitendo hicho, raia wa Saudia wamelaani vikali muamala huo usio wa kibinaadamu chini ya kauli mbiu ya 'Mtawala anamkandamiza raia wake' suala ambalo limewajumuisha pamoja raia wa taifa hilo kuwapinga watawala wa Aal-Saud. Habari kutoka Saudia zinaarifu kuwa, mashinikizo hayo ya fikra za walio wengi katika mitandao ya kijamii, imemlazimu Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud leo asubuhi kutoa amri ya kutiwa mbaroni mwanamfalme huyo na ambaye ni mmoja wa watu wa karibu wa mfalme wa sasa wa Saudia.

Raia masikini wa Saudia wanaotajwa kuwa ni watumwa na wanamfalme wa Saudia

Mfalme Salman ambaye kwa sasa anakabiliwa na mashinikizo ya wapinzani wa ndani kutokana na mgogoro wa kuwania madaraka, amekuwa akitekeleza ukandamizaji dhidi ya wapinzani na wakosoaji wake nchini humo na ni katika kujaribu kutuliza hali ya mambo ndipo ameamua kumtia mbaroni mwanamfalme huyo. Ama kwa upande wa nje, Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na hatua yake ya kuishambulia kijeshi Yemen.

 

 

 

Tags