Jul 24, 2017 14:59 UTC
  • Al Manar: Maandalizi ya kung'atuka Mfalme Salman Saudia yamekamilika

Gazeti la Lebanon la al-Manar limeandika kuwa, maandalizi ya mwisho ya kung'atuka mfalme mzee wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Al Saud kwa maslahi ya mwanaye Mohammad Bin Salman, yamekamilika.

Gazeti hilo limenukuu chanzo kimoja cha ndani ya utawala wa kifalme wa Aal-Saud kuhusiana na kukamilika maandalizi ya kung'atika Mfalme huyo wa Kiwahabi ambaye hali yake ya kiafya imeonekana kuwa mbaya na kwamba kujiuzulu huko kunafanyika kwa maslahi ya mwanaye.

Mfalme mtarajiwa, Bin Salman akiongea na Rais Trump

Kadhalika gazeti hilo la al-Manar limeandika zaidi kwamba, ili kuhakikisha anachukua madaraka, mrithi kijana wa kiti cha ufalme, Mohammad bin Salman amewapiga kalamu nyekundu mabinamu na washindani wake na kuwatia jela wengine kama ambavyo anaendelea kumzuilia Muhammad bin Nayef Al Saud, katika kifungo cha nyumbani.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha ndani ya utawala wa kifalme nchini Saudia, kiujumla hadi sasa Mohammad Bin Salman ndiye anayeshika madaraka ya ufalme na kwamba anafanya maandalizi ya kumpiga kalamu nyekundu pia Mutaib bin Abdullah bin Abdulaziz Al Saud, kutoka nafasi yake ya Kamanda wa Gadi ya Taifa. Habari za ndani zinasema kuwa, gari za wagonjwa na madaktari wa kigeni wamekuwa wakionekana wakiungua na kutoka kwenye makazi ya Mfalme Salman mwenye umri wa miaka 83, suala linaloashiria kuwa hali yake ya kiafya ni mbaya.

Mwanamfalme Bin Nayef aliyefungwa kifungo cha nyumban na Bin Salman

Kadhalika gazeti la al-Manar limeandika kuwa, baada ya kutangazwa Mohammad bin Salman kuwa Mfalme nchini humo, mwenendo wa mahusiano kati ya Saudia na Israel utaongezeka zaidi kama ambavyo mashirikiano ya utawala wa Kiwahabi wa Saudia na Tel Aviv yatawekwa wazi.

Al-Manar limeongeza kuwa, kuingia madarakani Mohammad Bin Salman kama mfalme wa Saudia, ni hatari sana na kutasababisha mgogoro mkubwa katika historia ya Saudia kutokana na ushindani mkali kati ya wanamfalme wa nchi hiyo.

Tags