Jul 25, 2017 08:10 UTC
  • Mfalme wa Saudia akabidhi uongozi wa nchi kwa mwanaye

Ofisi ya Mfalme wa Saudia imemtaka Mohammad bin Salman bin Abdulaziz Al Saud kijana na mrithi mpya wa kiti cha ufalme kushika hatamu za uongozi wa nchi, wakati wote wa safari nje ya nchi au kutokuwepo Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud.

Taarifa iliyotolewa Jumatatu ya jana na ofisi ya Mfalme ya nchi hiyo imesema kuwa, Mfalme  Salman bin Abdulaziz anaenda mapumziko nje ya Saudia.

Baadhi ya wanaharakati wa masuala ya kijamii wamefichua kuwa, mfalme huyo ni mgonjwa, na kwamba safari hiyo nje ya nchi ni katika maandalizi ya kumkabidhi madaraka mwanaye.

Gazeti la Rai al Youm limekinukuu chanzo kimoja katika ikulu ya mfalme wa Saudia kikielezea uwezekano wa mfalme wa sasa kung'atuka madarakani kwa maslahi ya mwanaye ndani ya kipindi cha miezi mitano ijayo.

Wanamfalme nchini Saudia

Baadhi ya magazeti ya nchi za Magharibi pia yameandika kuwa, kuna uwezekano Mfalme  Salman bin Abdulaziz akajiuzulu mwezi Septemba mwaka huu. Mapema jana pia gazeti la Lebanon la al-Manar liliandika kuwa, maandalizi ya mwisho ya kung'atuka mfalme huyo mzee wa Saudi Arabia, kwa maslahi ya mwanaye Mohammad Bin Salman, yamekamilika. Gazeti hilo lilifafanua zaidi kuwa, ili kuhakikisha anachukua madaraka, mrithi kijana wa kiti cha ufalme, Mohammad bin Salman amewapiga kalamu nyekundu mabinamu na washindani wake wote na kuwatia jela wengine kama ambavyo pia anaendelea kumzuilia Muhammad bin Nayef Al Saud, katika kifungo cha nyumbani.

Tags