Jul 28, 2017 07:35 UTC
  • Makumi ya Wapalestina watiwa nguvuni katika Msikiti wa Al-Aqsa

Askari wa utawala wa Kizayuni wa israel wamewavamia Wapalestina waliofanya mgomo wa kukaa kitako katika msikiti wa Al-Aqsa na kuwatia nguvuni zaidi ya watu mia moja.

Ofisi ya Waqfu katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu imetoa taarifa mapema leo na kueleza kwamba askari wa utawala haramu wa Israel wamewashambulia Wapalestina walioketi katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa kwa mabomu ya sauti na mabomu ya kutoa machozi. Katika hujuma hiyo, mbali na kuwajeruhi Wapalestina 115 na kuwatia nguvuni makumi ya wengine, askari wa utawala wa Kizayuni wameufunga tena msikiti wa Al-Aqsa na kuwazuilia waumini kusali ndani ya msikiti huo.

Wakati huohuo Mustafa Al-Barghouthi, Katibu Mkuu wa harakati ya ubunifu wa kitaifa ya Palestina ameashiria vitendo vya askari wa utawala ghasibu wa Israel vya kuwatusi na kuwapiga Waislamu wa Palestina na kutaka askari hao wapandishwe kizimbani na kuhukumiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Wapalestina wakisali Sala ya Ijumaa kwenye uwanja wa msikiti wa al-Aqsa

Al-Barghouthi amesema, Wapalestina wameibuka washindi baada ya mapambano ya siku 14 ya msikiti wa Al-Aqsa na kutoa wito kwa Wapalestina kujitokeza kwa wingi katika Sala ya Ijumaa ya leo kwenye kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.

Licha ya kila hatua iliyochukuliwa na adui Mzayuni ya kuwazuia Wapalestina wasiingie kwenye msikiti wa Al-Aqsa, maelfu ya Wapalestina jana waliingia kwenye uwanja wa msikiti huo mtukufu na kusali sala ya Alasiri. Hivi sasa askari wa Kizayuni wamewekwa katika hali ya tahadhari sambamba na Sala ya Ijumaa inayotazamiwa kusaliwa leo kwenye msikiti huo.

Tangu tarehe 14 ya mwezi huu wa Julai, askari wa utawala walikuwa wameifunga milango ya msikiti wa Al-Aqsa na kuweka mageti ya elektroniki kwa ajili ya kuingilia msikiti humo, lakini hatimaye wamelazimika kuyaondoa mageti hayo kutokana na malalamiko makubwa ya Wapalestina.../

 

Tags