Aug 09, 2017 02:37 UTC
  • Bahrain yaendelea kuwatia mbaroni wanaharakati wa kisiasa wakiwamo wanawake

Mkuu wa Taasisi ya Kisheria na Demokrasia (BIRD) nchini Bahrain, Ahmad al Wadai ametangaza kuwa, utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa umemhamishia jela Zainab Marhun mwanaharakati wa kisiasa wa nchi hiyo.

Al Wadai amesema kuwa, baada ya kumshikilia katika kituo cha polisi kwa masaa 48, askari wa utawala huo wamempeleka Zainab katika jela ya Isa ya nchi hiyo. Amefafanua zaidi kwamba hadi sasa jumla ya wanawake 10 wanaharakati wa kisiasa nchini, wanaendelea kuzuiliwa katika jela za serikali. Siku mbili zilizopita, askari wa Aal-Khalifa walifanya uvamizi katika nyumba kadhaa za raia wa kawaida wa eneo la al-Gharbiyyah, na kuwatia nguvuni watu wanane wasio kuwa na hatia.

Maandamano ya amani Bahrain

Aidha askari hao walivamia miji ya Karzakan, Dumistan na Malkiya na kuwatia mbaroni watu kadhaa akiwemo Zainab Marhun pamoja na mumewe. Zainab na mume wake ni wanaharakati wa kisiasa. Mwanamama huyo amekuwa akipinga ukandamizaji unaofanywa na utawala wa kiimla wa Aal-Khalifa nchini humo. Hata hivyo baada ya kumshikilia kwa saa 48 katika kituo cha polisi, Jumanne ya jana polisi walimpeleka jela. Bahrain ilikumbwa na malalamiko ya wananchi hapo mwezi Februari mwaka 2011, wakati raia wa taifa hilo walipomiminika mitaani wakilalamikia haki zao za msingi. Raia wa Bahrain wanataka uhuru, uadilifu na kuondolewa ubaguzi.

Tags