Harakati za kigaidi zashika kasi Sinai Kaskazini, Misri
Magaidi wenye mfungamano na kundi la kitakfiri la Daesh wamezisisha harakati zao katika eneo la Sinai Kaskazini nchini Misri licha ya askari usalama wa nchi hiyo kunzisha operesheni ya kuliandamana kundi hilo tangu miezi sita iliyopita.
Habari zinasema kuwa, polisi 18 wameuawa na wengine 7 kujeruhiwa baada ya magaidi kulenga kituo cha ukaguzi cha al Safaa katika mji wa al Arish huko kusini mwa Sinai Kaskazini. Baada ya shambulizi hilo jeshi la Misri lilifunga njia zote zinazoelekea kwenye baraza la mji wa al Arish.
Vyombo vya Misri vimetangaza kuwa, mapigano makali yameshuhudiwa katika eneo hilo na kwamba askari usalama wamewekwa katika hali ya tahadhari na kuzidisha usalama kwa kuanzisha vituo vya upekezi. Polisi ya Misri imesema magaidi 5 wameuawa katika mapigano hayo yaliyoendelea kwa masaa mawili.
Kundi la kigaidi linalojiita Ansaru Baitul Muqaddas lenye mfungamano na Daesh ambalo mwaka 2014 lilibadilisha jina lake na kujiita Jimbo la Sinai, limetoa taarifa likitangaza kua ndilo lililohusika na shambulizi dhidi ya kituo cha upekuzi cha al Shifaa. Taarifa hiyo imesema mashambulizi hayo yalianza kwa kulipulia gari lililokuwa lmetengwa mabomu na kuendelea kwa kushambulia maficho ya al Safaa na huko al Arish.
Alkhamisi iliyopita pia kundi hilo la kigaidi liliwaua askari 5 wa jeshi la Misri huko katika mji wa Rafah na kujeruhi makumi ya wengine.
Baada ya kupinduliwa serikali halali ya rais Muhammad Morsi Julai mwaka 2013 nchini Misri, eneo la jangwa la Sinai nchini Misri limekuwa maficho salama ya magaidi wa kundi la Daesh ambao wamekuwa tatizo kubwa kwa serikali ya Cairo kutokana na tabia ya jangwa ya eneo hilo na upana wake.
Japokuwa serikali ya Misri imefanya operesheni kadhaa kubwa katika eneo hilo kwa shabaha ya kuwaangamiza magaidi hao tangu miezi sita iliyopita lakini sababu kadhaa zikiwemo za ndani na za kieneo zimewawezesha magaidi kuzidisha harakati zao katika eneo hilo. Vilevile ushirikiano wa serikali ya Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha hali mbaya katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Kwa vyovyote vile mashambulizi na mauaji ya askari wa Misri katika eneo la Sinai Kaskazini yanazidi kuweka wazi udharura wa kuwepo juhudi za kimatafa za kukabiliana na makundi ya kigaidi hususan Daesh ambayo hayajui mipaka si ya kijiografia pekee bali hata mipaka ya utu na ubinadamu.