Oct 22, 2017 03:06 UTC

Polisi ya utawala wa Aal Khalifa unaendelea kukabiliana kwa njia mbalimbali na wanaharakati wa kisiasa huko Bahrain huku wapinzani nchini humo wakiendelea kila uchao kuwekwa jela kwa visingizio visivyo na msingi.

Katika fremu hiyo, Shirika la Amani kwa ajili ya Demokrasia na Haki za Binadamu la Bahrain limetangaza habari ya kutiwa mbaroni watu elfu 15 nchini humo katika kipindi cha miaka saba iliyopita. Takwimu zinaonyesha kuwa maelfu ya wanaharakati wa kisiasa katika miaka ya hivi karibuni walitiwa nguvuni huko Bahrain na kuwekwa korokoroni kwa muda katika jela za utawala wa Aal Khalifa; ambapo mwenendo huo umeshika kasi katika mwaka huu wa 2017. Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ambayo ni nchi ndogo zaidi katika Asia ya Magharibi ina wafungwa wengi wa kisiasa huku utawala ulioko madarakani wa Aal Khalifa ukiendelea kutekeleza siasa zake za ukandamizaji kwa kuungwa mkono na nchi za Magharibi. Ukandamizaji huo wa utawala wa Aal Khalifa umepelekea kuwepo wafungwa wa kisiasa zaidi ya elfu nne  katika jela za Bahrain. Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa karibu asilimia kumi ya wafungwa wa kisiasa huko Bahrain ni wanawake na watoto. Wimbi kubwa la utiaji mbaroni wanaharakati wa kisiasa huko Bahrain na kutolewa hukumu nzito dhidi yao ikiwemo hukumu ya kunyongwa  ni kinyume na kipengee cha kumi cha Hati ya Kimataifa kuhusu Haki za Binadamu na pia ni kinyume na kipengee cha sita cha Mkataba maalumu kuhusu haki za kiraia na kisiasa. 

Polisi wakitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya maandamano ya wapinzani  

Bahrain ilikumbwa na malalamiko na maandamano ya amani ya wananchi tangu Februari 14 mwaka 2011. Takwa kuu la wananchi wa Bahrain kwa utawala ulioko madarakani ni kuwa wanataka kuwepo madarakani serikali halali itakayochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, kukomeshwa ubaguzi, kufanyika marekebisho ya kisiasa, kuheshimiwa haki za binadamu, kutekelezwa uadilifu na uhuru na kuacha kuwa na utegemezi kwa nchi za Magharibi. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa badala ya kushughulikia matakwa ya wananchi wake, imeliweka katika ajenda yake ya kazi suala la kushadidisha ukandamizaji na kuwatia mbaroni kwa wingi raia wa nchi hiyo. Utawala wa Aal Khalifa umeshadidisha kuwatia mbaroni wapinzani wa kisiasa kwa kupanua wigo wa kamatakamata dhidi ya raia wa nchi hiyo. Utawala huo ulioko madarakani huko Bahrain unaendelea kutumia kila nyenzo, siasa na mbinu mbalimbali ili kuzima vuguvugu la harakati za ukombozi za wananchi na kuwafuta kabisa wapinzani katika uga wa kisiasa na kijamii wa nchi hiyo. Shughuli zozote za kisiasa zimepigwa marufuku huko Bahrain na hatua ya utawala huo ya kupasisha sheria kadhaa ina lengo la kuandaa mazingira ya kufuta kikamilifu haki za kisiasa za raia wa nchi hiyo.   

Ni muda sasa ambapo utawala wa Aal Khalifa umepasisha bungeni sheria ya kuwahukumu wapinzani wa kisiasa katika mahakama za kijeshi; sheria ambayo tayari imesainiwa na mfalme wa nchi hiyo na mkakati huo wa kuwafungulia mashtaka raia kwenye mahakama za kijeshi umewekwa katika ajenda ya kazi ya utawala huo. Mwaka 2015 pia bunge la nchi hiyo lilipasisha sheria kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi lengo kuu likiwa ni kuendeleza ukandamizaji dhidi ya wapinzani katika fremu ya hatua kubwa za ukandamizaji zinazotekelezwa na utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wapinzani nchini humo. Siasa zinazotekelezwa na utawala wa Bahrain zimeifanya nchi hiyo kuwa jela ya raia; hali ambayo imezitia wasiwasi mkubwa fikra za waliowengi duniani. Wakati huo huo kuchapishwa ripoti mbalimbali kuhusu hali mbaya waliyonayo wafungwa wa kisiasa huko Bahrain kunaakisi wasiwasi huo tajwa. 

Mwanzo wa vuguvugu la maandamano ya amani ya Wabahrain ya kutaka mageuzi 

 

 

 

Tags