Mar 23, 2016 08:10 UTC
  • Jordan yakataa kuwapa matibabu wakimbizi wa Syria

Maelfu ya wakimbizi raia wa Syria wamenyimwa huduma muhimu za matibabu na nchi jirani ya Jordan.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema wakimbizi hao wamekuwa wakipata wakati mgumu kupata huduma za matibabu walikokimbilia Jordan. Ripoti iliyotolewa leo Jumatano na Amnesty International imeonyesha kuwa, aghalabu ya raia laki 6 na elfu 30 wa Syria ambao wanatafuta hifadhi nchini Jordan hawapati matibabu licha ya kukabiliwa na maumivu makali na wengine kukumbwa na magonjwa ya kudumu. Kadhalika ripoti hiyo ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty imebainisha kuwa, idadi kubwa ya wakimbizi wa Syria waliozuiwa kuingia Jordan walipoteza maisha mipakani.

Watawala wa Jordan wamewawekea wakimbizi wa Syria vizingiti vingi vya kuingia nchini humo tangu mwaka 2012. Ripoti ya Amnesty International imesema kuwa, mwezi Julai mwaka jana, raia 14 wa Syria wakiwemo watoto wadogo watano ambao walikuwa na majeraha mabaya walizuiwa kuingia nchini Jordan, huku wanne kati yao wakiaga dunia mpakani baada ya kuzuiwa kukosa matibabu.

Itakumbukwa kuwa mnamo Septemba 30 mwaka uliopita wa 2015 na kwa ombi rasmi la serikali ya Syria, jeshi la Russia lilianzisha operesheni za mashambulio makali ya angani dhidi ya ngome za makundi ya kigaidi yaliyoko nchini Syria yanayoungwa mkono na nchi kadhaa za Kiarabu na za Magharibi ikiwemo Marekani.

Tags