Nov 16, 2017 08:09 UTC
  • Rais Erdoğan aichoma moyo Saudia, asisitiza kuendelea kuiunga mkono Qatar

Katika kile kinachonekana kuwa ni kuwachoma moyo viongozi wa Saudi Arabia katika mgogogro unaoendelea kati ya nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesisitizia uungaji mkono wake kwa Qatar.

Erdoğan ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Amiri wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani ambapo ameahidi kwamba, Ankara itaendelea kuiunga mkono kijeshi Qatar. Kadhalika katika mazungumzo hayo na kiongozi wa Qatar, kulitiwa saini makubaliano kadhaa kati ya pande mbili katika sekta za fedha, utalii na utafiti na masuala ya kijeshi.

Rais Erdogan akiwa na Amiri wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani

Aidha rais huyo wa Uturuki ametangaza kuisaidia Doha katika miradi ya maendeleo ukiwemo wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Kombe la Dunia la 2022 ambalo litafanyika nchini Qatar. Hii ni safari ya pili ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki nchini Qatar, tangu ulipoanza mgogoro kati ya Doha na Riyadh, yaani miezi mitano iliyopita. Katika mgogoro huo Uturuki ilitangaza kuisaidia Qatar suala ambalo lilitia doa mahusiano ya kisiasa kati ya Ankara na Riyadh.

Mfalme Salman wa Saudia

Katika uwanja huo hivi karibuni Rais Erdogan alikosoa vikali matamshi ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Mohammad Bin Salman kuhusu kile alichodai kuwa ni "Uislamu wa misimamo ya wastani." Akizungumza mjini Ankara, Erdogan alisema kuwa, Uislamu unaotajwa na mrithi huyo wa kiti cha ufalme nchini Saudia kuwa wa misimamo ya wastani ni Uislamu unaopigiwa debe na nchi za Magharibi. 

Tags