Watoto wa Kiiraqi; wahanga wakubwa wa ugaidi
Wizara ya Kazi na Masuala ya Jamii ya Iraq imetangaza kupitia taarifa iliyotoa kuwa inachunguza madai kwamba watoto waliokuwa wakilelewa katika kituo kimoja kinachosimamiwa na wizara hiyo katika mkoa wa Nainawa kaskazini mwa Iraq wameuzwa kwa kundi la kigaidi la Daesh.
Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa wahusika wote wa suala hilo la kuuza watoto watakabiliwa na mkono wa sheria kwa kuhusika na usaliti huo na kukiuka maadili ya kazi iwapo mashtaka dhidi yao yatathibitishwa.
Takwimu zilizotolewa na duru za ndani na kimataifa zinaonyesha kuwa katika miaka kadhaa ya karibuni watoto na wanawake wamekuwa wahanga wakuu wa vitendo vya ugaidi huko Iraq. Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Uwakilishi ya Umoja wa Mataifa Inayotoa Misaada kwa Iraq (UNAMI) zinaeleza kuwa, tangu mwaka 2014 yalipoanza mashambulizi ya kundi la Daesh huko Iraq na kufikia nusu ya kwanza ya mwaka jana wa 2017, watoto wa Kiiraqi 1,075 wameuawa katika matukio mbalimbali ya kigaidi nchini humo.
UNAMI imeongeza kuwa, watoto 1,130 pia wamejeruhiwa na kuwa vilema huku wengine 4,650 wakitengana na familia zao katika muda huo. Aidha watoto wa Kiiraqi zaidi ya milioni tano hivi sasa wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu.