Watu 27 wauawa katika hujuma ya kigaidi mjini Baghdad, Iraq
(last modified Mon, 15 Jan 2018 07:49:52 GMT )
Jan 15, 2018 07:49 UTC
  • Watu 27 wauawa katika hujuma ya kigaidi mjini Baghdad, Iraq

Watu wasiopungua 27 wameuawa na wengine zaidi ya 65 kujuruhiwa kufuatia mashambulizi mawili ya kigaidi katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Taarifa zinasema kuwa magaidi wawili waliokuwa wamejifunga mikanda iliyosheheni mabomu mapema leo wamejirupua katika Medani ya Al Tairan katika kati mwa Baghdad. Idadi ya waliopoteza maisha katika hujuma hiyo inatazamiwa kuongezeka kutokana na watu wengi kujeruhiwa vibaya. Hadi sasa hakuna kundi lololote lililodai kuhusika na hujuma hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq Saad Maan amesema magaidi wameshambulia eneo ambalo kwa kawaida vibarua hukusanyika wakitafuta kazi.

Mji mkuu wa Iraq umekuwa ukishuhudia utulivu wa wastani katika wiki za hivi karibuni tokea kundi la kigaidi la ISIS lifurushiwe mwezi Disemba kutoka maeneo yote ya Iraq liliyokuwa limeyakaliwa kwa mabavu.

Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al Abadi

Waziri Mkuu wa Iraq, Haydar al Abadi mwezi Disemba alitangaza rasmi kushindwa kundi la ISIS nchini humo na wakati huo huo kusisitiza kuwa, ushindi mkubwa zaidi ni kulindwa mshikamano na ardhi nzima ya Iraq na kuzuia kugawanyika vipande vipande nchi hiyo. 

Wanajeshi wa Iraq hivi sasa wanaendelea kupambana na mabaki ya magaidi wa ISIS ambao sasa wamechanganyika na raia wa nchi hiyo.