Jan 23, 2018 14:12 UTC
  • Utawala wa Bahrain waendelea kuwakandamiza wapinzani

Utawala wa kiimla wa Bahrain unaendelea kutumia wanajeshi wake kuwakandamiza wananchi wanaoandamana kwa amani wakitaka utawala wa demokrasia katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Katika tukio la hivi karibuni kabisa, mapema leo Jumanne, wanajeshi wa Bahrain walishambulia eneo la makazi ya raia na kuwatia mbaroni raia 25 akiwemo mwanazuoni wa Kiislamu.

Watu hao walikamatwa katika eneo la Diraz katika mji mkuu Manama na ni wafuasi wa Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni maarufu wa Kishia. Utawala wa Bahrain ulimpokonya uraia Sheikh Qassim mwezi Juni 2016 na kumfunga kifungo cha nyumbani tangu wakati huo hadi hivi sasa.

Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, utawala wa Bahrain umewakamata zaidi ya raia 11,000 wa nchi hiyo kwa tuhuma zisizo na msingi huku wengine wakipokonywa uraia na kufukizwa nchini humo.

Sheikh Isa Qassim

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema Bahrain ni nchi ndogo zaidi katika eneo la Asia Magharibi lakini ni nchi iliyo na idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa.

Ikumbukwe kuwa, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu.

Tags