Jeshi la Uturuki lashambulia kwa makombora maeneo ya makazi ya raia mjini Afrin, Syria
(last modified Wed, 14 Feb 2018 16:35:19 GMT )
Feb 14, 2018 16:35 UTC
  • Jeshi la Uturuki lashambulia kwa makombora maeneo ya makazi ya raia mjini Afrin, Syria

Katika kuendelea na operesheni za kijeshi za Uturuki kaskazini mwa Syria, jeshi la nchi hiyo limeshambulia kwa makombora maeneo ya makazi ndani ya mji wa Afrin.

Duru za habari mjini Afrin huko Syria zimeripoti kwamba katika mashambulizi hayo, watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa wakiwemo pia watoto wadogo. Hii ni katika hali ambayo vyombo vya habari nchini Syria vimeripoti kwamba wapiganaji wa Kikurdi wamezuia hujuma ya askari wa Uturuki na makundi ya wabeba silaha wanaoshirikiana na serikali ya Ankara, katika eneo la Douraka, mjini Afrin.

Wakazi wa Afrin wakiitaka jamii ya kimataifa kukomesha mauaji ya Uturuki dhidi yao

Aidha kumejiri mapigano makali kati ya wapiganaji hao wa Kikurdi na askari wa Uturuki katika kijiji cha Sheikh Khoras, mashariki mwa eneo la Bolbol, kaskazini mwa mji wa Afrin. Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumanne ya jana, taasisi ya haki za binaadamu yenye makao yake mjini London, Uingereza ilitoa ripoti mpya ikisema kuwa, hadi sasa jeshi la Uturuki limepoteza askari wake pamoja na wanamgambo wanaobeba silaha wapatao 202 katika operesheni za 'Tawi la Mzaituni' ambapo kwa mujibu wa ripoti hiyo 29 kati yao ni askari wa Uturuki. Katika sehemu nyingine, vyombo vya habari vya Syria vimetangaza kuwa, mamia ya wakazi wa eneo la Afrin hususan wanawake na watoto wamefanya maandamano Jumatano ya leo kulaani shambulizi la makombora la jeshi la Uturuki katika maeneo ya makazi katika eneo hilo.

Askari wa Uturuki wakiendeleza uchokozi katika eneo la Afrin

Wanawake hao wameitaka jamii ya kimataifa na asasi mbalimbali kufanya juhudi za kuhitimisha mashambulizi ya kichokozi ya jeshi la Uturuki katika eneo hilo. Kwa upande mwingine wapinzani wa serikali ya Uturuki wameendelea kukosoa siasa za Rais Recep Tayyip Erdoğan wa nchi hiyo na kusema kuwa ni siasa zilizofeli katika vita vyake kwenye eneo la Afrin, Syria.