Ndege ya jeshi ya Russia yaanguka Syria, yaua watu 32
Watu 32 wameuawa katika ajali ya ndege ya jeshi la Russia iliyoanguka nchini Syria.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa ndege hiyo ya mizigo aina ya Antonov-26 ilikuwa na abiria 26 na wahudumu 6 na kwamba imeanguka wakati ilipokuwa ikitua katika kituo cha anga cha Hmeimim katika mkoa wa Latakia ulioko magharibi mwa Syria.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, kuna uwezekano kwamba ajali hiyo imetokana na matatizo ya kiufundi.
Hii ni mara ya pili ndege aina ya Antonov-26 ya usafiri wa kijeshi inayoweza kubeba abiria 38 na kilo 5,500 za mizigo, kuanguka nchini Syria. Ndege nyingine ya aina hiyo ya Syria alianguka wakati ilipokuwa ikitua kwenye uwanja wa ndege wa Abu al-Duhur huko Idlib Januari 2015.
Russia inatumia kituo cha jeshi la anga cha Hmeimim katika mkoa wa Latakia na kile cha baharini katika bandari ya Tartus nchini Syria katika mapambano yake dhidi ya makundi ya kigaidi.
Majeshi ya Russia yako nchini Syria kwa ombi la serikali ya Damascus.