Russia: Hakuna shambulizi la silaha za kemikali lililofanyika Duma, Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42870-russia_hakuna_shambulizi_la_silaha_za_kemikali_lililofanyika_duma_syria
Kituo cha uangalizi wa kijeshi wa jeshi la Russia nchini Syria kimetangaza kwamba, hakuna shambulizi lolote la silaha za kemikali lililofanyika karibu na mji wa Duma eneo la Ghouta Mashariki katika viunga vya Damascus, mji mkuu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 09, 2018 09:48 UTC
  • Russia: Hakuna shambulizi la silaha za kemikali lililofanyika Duma, Syria

Kituo cha uangalizi wa kijeshi wa jeshi la Russia nchini Syria kimetangaza kwamba, hakuna shambulizi lolote la silaha za kemikali lililofanyika karibu na mji wa Duma eneo la Ghouta Mashariki katika viunga vya Damascus, mji mkuu wa nchi hiyo.

Awali duru za habari kutoka kwa magaidi ziliripoti kwamba Jumamosi iliyopita ndege ya jeshi la Syria ilifanya shambulizi la silaha za kemikali katika eneo hilo ambapo kutokana na hujuma hiyo watu 75 walipoteza maisha na makumi ya wengine kujeruhiwa. Hata hivyo Yuri Yevtushenko, mkuu wa kituo hicho cha uangalizi wa kijeshi amesema kuwa, madai yote ya Wamaghribi dhidi ya jeshi la serikali ya Syria kwamba imetumia silaha za kemikali mjini Duma, ni kadhia ya kubuni tu na wala haina ukweli wowote.

Sargey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia

Kadhalika mkuu huyo wa kituo cha uangalizi wa kijeshi wa jeshi la Russia nchini Syria amesisitiza kuwa, Moscow ipo tayari kutuma wataalamu wake kwa ajili ya kukusanya taarifa kuhusiana na suala hilo ili kufichua madai hayo bandia. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa, madai kwamba jeshi la Syria limetumia silaha za kemikali yametolewa kwa lengo la kufunika jinai za makundi ya kigaidi na kadhalika kuhalalisha mashambulizi yao dhidi ya nchi hiyo. Kadhalika Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia sambamba na kutahadharisha juu ya aina yoyote ya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria kwa kutumia ripoti za uongo na za kubuniwa, imesema kuwa hatua hiyo itakuwa na matokeo mabaya.

Silaha za kemikali za magaidi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria pia imetangaza kuwa, tuhuma za uongo za baadhi ya nchi dhidi ya serikali ya Damascus kuhusiana na silaha za kemikali, zinalenga kuendeleza uhai wa makundi ya kigaidi nchini Syria. Kufuatia madai hayo, vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na vinavyoyaunga mkono makundi ya kigaidi, vimeanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya serikali ya Syria. Inafaa kuashiria kuwa, hadi sasa makundi ya kigaidi na ya Kiwahabi yameshafanya jinai nyingi nchini Syria, ikiwemo ya kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia.