Japan yaipinga Marekani, yasema haitahamishia ubalozi wake Beitul-Muqaddas
Waziri Mkuu wa Japan amesisitiza kuwa, nchi yake haitaungana na Marekani katika uamuzi wake na kwamba, haitahamishia ubalozi wake katika mji wa Beitul-Muqaddas
Shinzo Abe amesema hayo mjini Ramallah Palestina katika mazungumzo yake na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kusisitiza kwamba,ubalozi wa Japan utaendelea kubakia huko Tel Aviv na kwamba, Tokyo haina mpango kabisa wa kuhamishia ubalozi wake huko Quds.
Waziri Mkuu wa Japan jana aliwasili huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu akitokea Jordan.
Baadaye leo, Waziri Mkuu huyo wa Japan anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Sisitizo hilo la Japan la kubakisha ubalozi wake huko Tel Aviv linahesabiwa kuwa pigo jingine kwa Marekani ambayo imekuwa ikihaha kuyakinaisha mataifa mengine yaungane nayo katika uamuzi wake wa kuitambua Beitul-Muqaddas kuwa ndio mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 6 Disemba mwaka jana Rais Donald Trump wa Marekani alichukua hatua ambayo ni kinyume na maazimio ya kimataifa ya kuitangaza Quds Tukufu kuwa eti mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Aidha rais huyo wa Marekani alitangaza kuwa serikali ya Washington imeanzisha mchakato wa kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel Aviv. Uamuzi huo wa Trump ulilaaniwa na unaendelea kulaaniwa kila pembe ya dunia hususan katika ulimwengu wa Kiislamu.