Ripoti: Marekani imekuwa ikipigana bega kwa bega na Saudia nchini Yemen
Gazeti moja la nchini Marekani limefichua kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wamekuwa wakishirikiana moja kwa moja na Saudi Arabia katika vita nchini Yemen
Toleo la mtandaoni la gazeti la New York Times jana lilifichua kuwa, wanajeshi wa kikosi maalumu cha jeshi la Marekani kinachojulikana kwa jina la Green Berets wanashiriki kwa siri katika vita vya Yemen wakipigana bega kwa bega na wanajeshi wa Saudi Arabia.
Gazeti hilo la New York Times limeongeza kuwa, licha ya jeshi la Marekani kujaribu kujiepusha kuingia moja kwa moja katika vita vya Yemen kwa miaka mingi sasa, lakini mwishoni mwa mwaka jana lilituma timu ya makumi ya wanajeshi wa kikosi chake maalumu cha Green Berets katika mpaka wa Saudi Arabia na Yemen.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Marekani, hata huko nyuma, wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon ilikuwa ikikiri jambo hilo ingawa kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kwa kutumia maneno kama tunashirikiana kwa kiwango cha chini na Saudi Arabia katika vita vya Yemen. Hata hivyo maneno hayo ya Pentagon yanakinzana na uhalisia wa mambo.
Gazeti la New York Times limeongeza kuwa, Pentagon imekuwa ikidai kuwa inashirikiana na Saudi Arabia katika vita vya Yemen kwa kiwango kidogo cha kujaza mafuta ndege za kivita, masuala ya kilojistiki na kubadilishana taarifa za kijasusi, lakini hatua ya kikosi cha nchi kavu cha jeshi la Marekani ya kutuma wanajeshi wake katika mpaka wa Saudi Arabia na Yemen ni ushahidi kuwa Pentagon inashiriki moja kwa moja kwenye vita hivyo na haitoi misaada midogo midogo tu kwa Saudia.