Saudia kuwatimua wahajiri laki tano raia wa Ethiopia
Saudi Arabia imekubali ombi la Ethiopia la kuwaachia huru wahajiri wapatao elfu moja raia wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, lakini imesisitiza kuwa itawafukuza nchini humo malaki ya wahajiri wengine wa nchi hiyo ya Kiafrika.
Riyadh imekubali kuwaachia huru raia hao wa Ethiopia wakiwemo wanawake 100, ambao ilikuwa ikiwazuilia, kufuatia ombi la Waziri Mkuu Abiy Ahmed. Hata hivyo utawala wa Riyadh haujatoa maelezo yoyote kuhusu tuhuma zilizokuwa zikiwabili wahajiri hao.
Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye aliitembelea Saudia katika safari yake ya kwanza nje ya bara Afrika mwishoni mwa wiki hii, ameitaka serikali ya Riyadh iwape ulinzi na kuwadhaminia usalama wahajiri wa nchi hiyo ya Kiafrika wanaoshi nchini humo.

Utawala wa Aal-Saud upo mbioni kuwafukuza nchini humo wahamiaji laki tano wa Kiafrika, unaodai kuwa ni wahajiri haramu.
Tayari Riyadh imewatimua nchini humo wahajiri laki moja na elfu 60 wa Ethiopia kufikia sasa.