Hamid Karzai: Marekani ilinishinikiza nivunje mahusiano na Iran
Rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai amesema kuwa, katika kipindi cha uongozi wake Marekani ilimshinikiza sana ikimtaka akate uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini hakukubali kufanya hivyo na amesisitiza kuwa Washington imewafanyia hiyana kubwa raia wa Afghanistan na eneo lote la Mashariki ya Kati.
Karzai ameongeza kwamba, stratijia zinazotekelezwa sasa na viongozi wa Marekani Afghanistan na katika eneo lote la Mashariki ya Kati, ni stratijia ya vita na kwamba mwenendo huo ndio unaochafua usalama katika eneo hilo. Rais wa zamani wa Afghanistan amesema haifai kuwaamini Wamarekani na kuongeza kuwa madai ya kutetea demokrasia, uhuru na usalama wa raia wa Afghanistan na nchi nyingine za eneo hili ni maneno matupu yasiyo na msingi na kwamba mambo hayo hayana thamani yoyote katika imani ya viongozi wa Washington.
Amesema kuwa, badala ya Wamarekani kupambana na ugaidi na nchi zinazounga mkono ugaidi, wanawashambulia na kuwaua raia wa Afghanistan ambao kimsingi ndio wahanga wakubwa wa ugaidi na kwamba uwepo wa askari wa Marekani nchini humo umevuruga usalama wa taifa hilo kuliko wakati mwingine.
Akiashiria mashinikizo ya Marekani kwa ajili ya kuizuia serikali ya Kabul kupanua uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, rais huyo wa zamani wa Afghanistan amesema, katika kipindi cha urais wake Wamarekani na kwa namna ya wazi walikuwa wakimtaka akate uhusiano wa nchi yake na Iran.
Ameenda mbali zaidi na kusema kuwa, nafasi chanya ya Iran katika maendeleo na kusimamia amani ni yenye umuhimu mkubwa kwa Afghanistan na kuongeza kuwa, lau kama si misimamo yenye kutumia mantiki na chanya ya Tehran, basi hali ya Afghanistan ingekuwa mbaya zaidi kuliko ilivyo kwa sasa.