Wanajeshi wa Israel wamewaua shahidi Wapalestina 180 katika maandamano
(last modified Sat, 25 Aug 2018 07:04:12 GMT )
Aug 25, 2018 07:04 UTC
  • Wanajeshi wa Israel wamewaua shahidi Wapalestina 180 katika maandamano

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa tokea yaanze 'Maandamano ya Haki ya Kurejea' Machi 30 mwaka huu wa 2018, Wapalestina 180 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wizara ya Afya ya Palestina ilitoa taarifa Ijumaa na kusema tokea kuanze wimbi hilo jipya la maandamano miili 171 ya mashahidi Wapalestina imefikishwa katika vituo vya afya vya Ghaza na miongoni mwao walikuwemo watoto na wanawake 27 na wafanyakazi watatu wa kutoa huduma za afya pamoja na mwandishi habari. Aidha miili mingine 9 ya mashahidi Wapalestina inashikiliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kwa msingi huo idadi ya mashahidi wote hadi sasa ni 180.

Aidha Wizara ya Afya ya Palestina imesema katika maandamano hayo, Wapalestina 18,000 wamejeruhiwa na wengine 423 wako katika hali mahututi.

Mfanyakazi wa huduma za afya aliyejeruhiwa na wanajeshi wa Israel katika maandamano ya amani huko Ghaza

Tarehe 30 Machi, sambamba na kutimia mwaka wa 42 wa Siku ya Ardhi, maelfu ya Wapalestina wakazi wa Ukanda wa Gaza walianzisha maandamano ya amani ya "Haki ya Kurejea" ili kutilia mkazo azimio nambari 194 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo kifungu chake cha 11 kinaashiria haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea kwenye ardhi zao. Maandamano hayo ya amani yamekuwa yakifanyika kila Ijumaa katika mpaka wa Ghaza na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kukandamizwa kwa mkono wa chuma na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tags