Russia: Magaidi nchini Syria wamejiandaa kufanya shambulio la silaha za kemikali
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia ametangaza kuwa magaidi walioko nchini Syria wamejiandaa kufanya shambulio la silaha za kemikali katika kipindi cha siku hizi mbili.
Meja Jenerali Igor Konashenkov amesema magaidi wamekusudia kufanya shambulio kwa kutumia silaha za kemikali katika mkoa wa Idlib nchini Syria.
Akiashiria taarifa zilizopatikana kutoka kituo cha Russia cha maridhiano baina ya pande zinazopigana nchini Syria, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia ameongeza kuwa kundi moja la wataalamu wanaozungumza Kiingereza limeelekea mkoani Idlib kutoa mafunzo kwa magaidi ya utumiaji wa silaha zinazobeba mada za klorini.
Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia, shambulio hilo limepangwa kufanywa katika eneo la Kafr Zita na kwamba magaidi tayari wameshatuma eneo hilo kundi moja la raia wa Syria kutoka kaskazini mwa Idlib kwa ajili ya kutengeza filamu ya kuonyesha kuwa watu hao wameathirika kutokana na shambulio la silaha za kemikali.
Konashenkov amefafanua kuwa lengo la njama hiyo ni kulituhumu jeshi la Syria kuwa ndilo lililohusika na shambulio hilo ili kuhalalisha shambulio jengine la madola ajinabi dhidi ya ngome za jeshi la Syria.
Siku ya Jumamosi pia msemaji huyo wa Wizara ya Ulinzi ya Russia alitangaza kwamba Marekani, Uingereza na Ufaransa zimeshajiandaa kufanya shambulio jengine jipya dhidi ya Syria na kwamba manowari ya Marekani ya USS The Sullivans na ndege za kivita aina ya Rockwell B-1 Lancer zimeshawasili eneo la Ghuba ya Uajemi na kwenye kituo cha anga cha nchi hiyo kilichoko Qatar.../