OIC yataka kusitishwa ujenzi wa vitongozi vya walowezi wa Kizayuni
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa wito wa kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imezitaka asasi za kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za maana za kusitisha ujenzi haramu wa vitingoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala haramu wa Israel.
Yousef Al-Othaimeen, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amelaani mpango wa utawala ghasibu wa Israel wa kujenga nyumba 1000 huko Quds inayokaliwa kwa mabavu na kutangaza kuwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa ujenzi wa vitongoji hivyo unaofanywa na Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Beitul-Muqaddas si wa kisheria.

Aidha Katibu Mkuu wa OIC ameongeza kuwa, ujenzi huo unakinzana wazi na bayana na maazimio ya kimataifa na ni kukanyaga haki za taifa la Palestina.
Israel inaendelea na ujenzi huo wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni licha ya kwamba, mwaka 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 lililoutaka utawala ghasibu wa Israel kusitisha mara moja na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina unafanyika kwa shabaha ya kubadili muundo wa kijamii na kijiografia wa ardhi ya Palestina.