Amnesty International yalaani kifungo cha maisha dhidi ya Sheikh Ali Salman
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49286-amnesty_international_yalaani_kifungo_cha_maisha_dhidi_ya_sheikh_ali_salman
Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limetoa taarifa likilaani hukumu ya kifungo cha maisha iliyotolewa na watawala wa Bahrain dhidi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya al-Wifaaq.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 05, 2018 07:13 UTC
  • Amnesty International yalaani kifungo cha maisha dhidi ya Sheikh Ali Salman

Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limetoa taarifa likilaani hukumu ya kifungo cha maisha iliyotolewa na watawala wa Bahrain dhidi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya al-Wifaaq.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu duniani, limesema kwamba hukumu hiyo ya kifungo cha maisha iliyotolewa dhidi ya Sheikh Ali Salman ni ishara hatari ya kuendelea siasa za ukandamizaji na zisizo za kisheria za utawala wa Manama dhidi ya wanaharakati wa masuala ya kiraia wa Bahrain. Kikao cha nne cha mahakama ya rufaa kuhusiana na kesi ya Sheikh Salman na wabunge wa zamani wa Bahrain kutoka Jumuiya ya al-Wifaaq kilifanyika jana Jumapili ambapo mbali na hukumu ya Sheikh Salman, hukumu ya kuachiliwa huru wabunge hao ilifutiliwa mbali na wote watatu wakapewa vifungo vya maisha jela.

Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al-Wifaq ya nchini Bahrain

Sheikh Ali Salman mmoja wa viongozi wa Kishia nchini Bahrain alikamatwa mwaka 2014 na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela mwezi Julai mwaka 2015, lakini baadaye mahakama ya rufaa ya nchi hiyo ikaongeza muda huo hadi miaka 9 ambapo  katika hukumu ya hivi karibuni imebadilisha hukumu yake ya awali na kumpa mwanazuoni huyo mashuhuri wa Bahrain kifungo cha maisha. Hukumu hiyo imetolewa siku moja baada ya mfalme wa Bahrain kukutana na kuzungumza na mfalme mwenzake wa Saudi Arabia jambo linalobainisha wazi ushirikiano mkubwa uliopo baina ya watawala wa nchi mbili hizo za kifalme katika kuwakandamiza wapinzani wao wa kisiasa. Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati za mapinduzi ya wananchi tokea tarehe 14 Februari 2011. Wananchi hao ambao wanapigania uhuru, uadilifu, kuondoleawa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi, wamekuwa wakikabiliwa na mkono wa chuma na ukandamizaji wa kupindukia kutoka kwa watawala vibaraka wa nchi hiyo ambao wanaungwa mkono kijeshi na askari wa Saudia na askari usalama wa Imarati.