Onyo la Ansarullah kwa kutoheshimiwa usitishaji vita nchini Yemen
(last modified 2016-04-13T06:56:36+00:00 )
Apr 13, 2016 06:56 UTC
  • Onyo la Ansarullah kwa kutoheshimiwa usitishaji vita nchini Yemen

Siku chache zikiwa zimepita tangu kutangazwa kusimamishwa vita nchini Yemen, msemaji wa harakati Ansarullah ya nchi hiyo amesema kuwa, iwapo makubaliano hayo hayataheshimiwa, basi fursa za kufanikiswa mazungumzo ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo zitapotea.

Muhammad Abdus Salaam amesema, kitendo cha muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia cha kuendelea kufanya mashambulizi katika makazi ya watu huko Yemen ni uvunjaji wa wazi wa makubaliano hayo na inabidi kikomeshwe mara moja. Siku ya Jumapili ya tarehe 10 Aprili, kuliundwa kamati za kieneo za kusimamia mchakato wa kusimamisha mapigano katika mikoa 6 ya Jawf, Maarib, Taiz, Baydha, Shab'wah na adh Dhali'. Kamati hizo za kieneo zina kazi ya kusimamia usitishaji vita katika maeneo ya mapigano, kuzuia kuchukuliwa hatua yoyote ya kijeshi pamoja na kufungua njia kwa ajili ya kuusaidia Umoja wa Mataifa kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa nchi hiyo. Wakati huo huo kiongozi mwingine mwandamizi wa Baraza la Kisiasa la harakati ya Ansarullah amesema kuwa, harakati hiyo inataka mapigano yasimamishwe kikamilifu nchini Yemen. Amesema, harakati hiyo imelegeza kamba katika masuala mbalimbali ili kufanikisha jambo hilo. Hata hivyo, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukivunja mara kwa mara makubaliano hayo baada ya kuona umeshindwa kufikia malengo yake ya kuivamia nchi hiyo ya Kiarabu. Makubaliano hayo tete ya kusimamisha vita huko Yemen yalianza kutekelezwa usiku wa kuamkia tarehe 11 Aprili. Ikumbukwe kuwa tarehe 18 mwezi huu wa Aprili, Kuwait itakuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani ya Yemen. Hii ni katika hali ambayo mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen amesema, kuna udharura wa kuheshimiwa makubaliano hayo ingawa Saudia bado inang'ang'ania kuyavunja. Katika siku ya pili tu ya kuanza kutekelezwa makubaliano hayo, ndege za Saudia zilifanya mashambulizi katika mikoa ya Saada na Taiz. Brigedia Jenerali Sharaf Luqman, msemaji wa jeshi la Yemen amesema, jeshi la nchi hiyo lina haki ya kujibu mashambulizi hayo ya Saudia lakini itambulike vyema kuwa, kuendelea kuvunja makubaliano hayo ni kwa madhara ya mazungumzo ya amani ya nchini Kuwait. Wakati huo huo Umoja wa Mataifa na nchi nyingi duniani, zimepokea vizuri makubaliano ya kusimamisha vita na kutaka kukomeshwe vitendo vyote vya kuvunja makubaliano hayo. Nchi hizo aidha zimetaka wananchi madhlumu wa Yemen walindwe na kuepushwa nchi hiyo kutumbukia kwenye janga la kibinadamu. Kwa upande wake, Amir Abdollahian, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya Kiarabu na Kiafrika amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu daima inafanya juhudi za kuhakikisha kuwa kunafuatwa njia za kisiasa za kutatua mgogoro wa Yemen. Ametaka kuheshimiwa makubaliano ya kusitisha vita na ameutaka Umoja wa Mataifa uzilazimishe nchi zilizoizingira Yemen ziache mara moja kufanya hivyo. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, uvamizi wa kijeshi wa Saudia nchini Yemen umevuruga usalama wa nchi za eneo hili na umeandaa uwanja wa kuongezeka vitendo vya kigaidi na kusababisha hasara kubwa za roho na mali za watu wa eneo hili zima.

Tags