Dec 31, 2018 13:37 UTC
  • Afungwa miaka mitano jela kwa kusema tu Wayemen wanaonewa

Ikiwa ni kuendeleza dhulma yake isiyo na kifani, utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa wa nchini Bahrain umemuhukumu kifungo cha miaka mitano jela, mwanaharakati maarufu Nabil Rajab kwa kuandika tu katika mtandao wa Twitter kwamba Wayemen wanadhulumiwa na muungano vamizi wa Saudi Arabia.

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, Nabil Rajab amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela na mahakama moja ya Bahrain kwa sababu ya kuwatetea wananchi wa Yemen kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Katika ujumbe wake kupitia mtandao huo wa kijamii, mwanaharakati huyo wa haki za binadamu alilaani mauaji wanayofanyiwa wananchi wa Yemen na muungano wa baadhi ya nchi za Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia.

Mabaki ya basi la shule nchini Yemen baada ya kushambuliwa kinyama na ndege za muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia

 

Mahakama ya rufaa ilitoa hukumu hiyo mwezi Juni mwaka huu wa 2018 lakini mwanaharakati huyo alifungua kesi katika mahakama ya juu zaidi na ilikuwa imepangwa leo tarehe 31 Disemba ombi lake hilo lisikilizwe.

Kabla ya hapo mashirika 127 ya haki za binadamu yalitoa taarifa ya pamoja yakiutaka utawala wa kidikteta wa Bahrain umuachilie huru mara moja mwanaharakati huyo.

Kamati ya kimataifa ya haki za binamu ilielezea wasiwasi wake kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Bahrain na kusema kuwa, mazingira ya waharakati wa kisiasa nchini humo imezidi kuwa mbaya mwaka 2018.

Tags