Mkutano wa Moscow; mwanzo wa mazungumzo jumuishi baina ya Waafghani
Hamid Karzai, Rais wa zamani wa Afghanistan na viongozi wa baadhi ya vyama vya nchi hiyo wanakutana na kundi la wanamgambo wa Taliban huko Moscow, mji mkuu wa Russia, ikiwa ni hatua moja mbele katika fremu ya kuanza mazungumzo jumuishi baina ya Waafghani.
Hamid Karzai ambaye amealikwa kushiriki katika mkutano huo anaamini kuwa, mkutano wa amani wa Moscow Kuhusu Afghanistan unaweza kuandaa mazingira ya kuhitimishwa vita na kurejea amani na uthabiti nchini Afghanistan. Mbali na Karzai, kuna shakhsia kadhaa watajika kisiasa na wenye ushawishi nchini Afghanistan akiwemo Muhammad Muhaqiq, Karim Khalili, Atta Muhammad Nur, Mohammad Hanif Atmar na Gulbuddin Hekmatyar ambao nao wanashiriki katika mkutano huo wa siku mbili wa mjini Moscow ulioanza Jumanne ya jana.
Kwa kuzingatia kwamba, kundi la wanamgambo wa Taliban limekataa kufanya mazungumzo na serikali ya Afghanistan, mkutano wa Moscow unahesabiwa kuwa fursa muhimu ya kukutana na kufanya mazungumzo kwa mara ya kwanza baina ya wawakilishi wa kundi hilo na shakhsia muhimu wa kisiasa na ambao wana taathira muhimu kwa matukio ya Afghanistan.
Licha ya kuwa serikali ya Kabul imeupinga mkutano huo wa Moscow na inasisitiza juu ya kufanyika mazungumzo hayo kwa usimamizi wake, lakini washiriki wa mkutano wa Moscow ambao wanatoka katika makundi, kaumu na mirengo mbalimbali ya kisiasa na hata kutoka katika makundi ya kijihadi, wana matumaini kwamba, mazungumzo ya ana kwa ana baina ya pande zinazozozana katika mgogoro wa Afghanistan yataandaa mazingira mwafaka na anga ya lazima kwa ajili ya kufanyika mazungumzo baina ya serikali ya Kabul na kundi la wanamgambo wa Taliban.
Hasa kwa kutilia maanani kwamba, vyovyote itakavyokuwa mwisho wa siku ni serikali ya Afghanistan ndio ambayo inapaswa kutiliana saini hati ya makubaliano ya amani na wanamgambo wa Taliban.
Ihsan Taheri, msemaji wa Baraza Kuu la Amani nchini Afganistan amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na mtandao wa habari wa Parstoday kwamba:
Baraza Kuu la Amani la Afghanistan daima limekuwa likilitaka kundi la wanamgambo wa Taliban kuheshimu wito wa kutaka amani wa wananchi wa nchi hiyo na litangaze utayari wake wa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Kabul.
Hata kama Marekani imekuwa ikifuatilia siasa za kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la Taliban na hivi karibuni ilifanya duru ya sita ya mazungumzo na wanamgambo hao huko Doha mji mkuu wa Qatar, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia daima zimekuwa zikifanya juhudi za kulikinaisha kundi la wanamgambo hao ili lifanye mazungumzo na serikali ya Kabul.
Hatua ya Iran ya kuwaalika baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa Taliban hapa Tehran, ilikuwa na taathira kwa kundi hilo kukaa katika meza moja ya mazungumzo na mirengo mingine na shakhsia wa kisiasa wa Afghanistan.
Hii ina maana kuwa, Mkutano wa Moscow Kuhusu Afghanistan ni matunda ya juhudi zote za kieneo kwa ajili ya kusaidia kusukuma mbele gurudumu la mwenendo wa amani wa nchi hiyo.
Vahid Muzhdeh, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Idhaa ya Dari ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba:
Hapana shaka kuwa, nchi jirani na Afghanistan ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zina nafasi muhimu katika kutatuliwa matatizo ya nchi hiyo. Hivyo basi, kuna haja ya kuzitaka zaidi nchi hizo zisaidie mwenendo wa mazungumzo ya amani nchini Afghanistan.
Alaa kulli haal, kundi la wanamgambo wa Taliban, nalo limefikia natija hii kwamba, si tu kwamba, wananchi wa Afghanistan wamechoka na vita, bali hata kundi hilo nalo haliwezi kutwaa madaraka ya nchi hiyo kupitia njia ya utumiaji mabavu na umwagaji damu.