Kuakisiwa kusalimu amri viongozi wa Misri mbele ya Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i5158-kuakisiwa_kusalimu_amri_viongozi_wa_misri_mbele_ya_saudi_arabia
Wananchi wa Misri wametaka kung'olewa madarakani serikali ya al Sisi katika kulalamikia hatua ya serikali hiyo ya kuipatia Saudia visiwa visiwa vya Tiran na Sanafir vilivyoko katika bahari Nyekundu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 16, 2016 08:15 UTC
  • Kuakisiwa kusalimu amri viongozi wa Misri mbele ya Saudi Arabia

Wananchi wa Misri wametaka kung'olewa madarakani serikali ya al Sisi katika kulalamikia hatua ya serikali hiyo ya kuipatia Saudia visiwa visiwa vya Tiran na Sanafir vilivyoko katika bahari Nyekundu.

Wafanya maandamano wa Misri huku wakipiga nara ya "wananchi wanataka kung'olewa utawala ulioko madarakani, kung'olewa utawala mbaya wa wanajeshi", walishiriki maandamano makubwa ili kupinga hatua hiyo ya serikali ya Cairo, ambapo waliwataja wauzaji wa ardhi ya nchi hiyo kuwa ni wahaini.

Mfalme Salman wa Saudia katika safari yake hivi karibuni huko Misri alisaini makubaliano kadhaa ya kiuchumi na kisasa na nchi mwenyeji; ambapo kwa mujibu wake moja ya masuala yaliyofikiwa kwenye makubaliano hayo ni kuhusu kuchorwa upya mipaka ya baharini kati ya nchi mbili hizo. Makubaliano hayo yanaeleza kuwa, visiwa vya Tiran na Sanafir vimetambuliwa kuwa ni sehemu ya ardhi ya Saudi Arabia.

Serikali ya Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri imetetea hatua yake ya kuipatia Saudi visiwa viwili hivyo kufuatia ziara ya hivi majuzi ya Mfalme wa nchi hiyo huko Cairo, kitendo ambacho kimewakasirisha sana wananchi wa Misri. Serikali ya Misri imeeleza kuwa nchi hiyo haijasalimisha ardhi yake, bali imewarejeshea Wasaudia haki yao.

Uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Cairo kuhusiana na suala hilo umetekelezwa katika hali ambayo Misri huko nyuma iliwahi kutangaza kuwa viongozi wa Misri wanapasa kuwa na taarifa kuhusu meli yoyote inayotaka kutia nanga katika lango la Tiran. Mwaka 1906 Misri ilisaini mkataba wa kuainisha mipaka yake ya mashariki kati yake na serikali ya Othmania; na kwa mujibu wa mkataba huo visiwa hivyo viwili vilitambuliwa kuwa sehemu ya ardhi ya Misri.

Kisiwa cha Sanafir kina ukubwa wa kilomita mraba 33 kilichopo katika lango la Tiran, huku kikitenganishwa na Ghuba ya Aqabah katika bahari Nyekundu.

Wakati huo huo baadhi ya duru za habari zinaarifu kuwa, utendaji wa Rais al Sisi khususan hatua yake ya kuuza ardhi ya Misri, imekabiliwa na upinzani ndani ya jeshi la Misri pia. Katika fremu hiyo tovuti ya habari ya al Shaab ya Misri imeashiria habari kuhusu kuzimwa njama ya mapinduzi iliyopangwa na baadhi ya maafisa wa jeshi wa ngazi ya juu wa Misri dhidi ya Rais Abdel Fattah al Sisi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mahmoud Rafaat Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Sheria na Uhusiano wa Kimataifa cha Misri amefichua kuwa idara ya itelijinsia ya jeshi la Misri tangu siku mbili zilizopita imeanza kuwakamata baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi la nchi hiyo, ambapo baadhi ya maafisa hao walitiwa mbaroni wakiwa sehemu zao za kazi.

Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Sheria na Uhusiano wa Kimataifa cha Misri ameeleza kuwa kamatakamata hiyo huenda inahusiana na baadhi ya matukio na tetesi za siku kadhaa zilizopita kwamba, baadhi ya maafisa wa jeshi lal Misri wamepanga njama ya kumpindua Rais Abdel Fattah al Sisi katika kupinga hatua yake ya kuvigawa visiwa viwli vya Tiran na Sanafir kwa Saudi Arabia. Hii ni katika hali ambayo siku kadhaa zilizopita Taasisi kwa jina la "Mrengo wa Kiraia" ya Misri ilieleza kuwa Rais wa nchi hiyo hana haki ya kuigawa ardhi ya Misri kwa Saudia. Hamdan Sabahi mgombea wa zamani wa kiti cha urais huko Misri amelaani hatua hiyo ya serikali ya Cairo. Akimhutubu Rais al Sisi, Sabahi amesisitiza kuwa kwa mujibu wa kipengee cha kwanza na cha 151 cha katiba ya Misri, Rais hana haki ya kufumbia macho ardhi yanchi na kwamba haruhusiwi kwa hali yoyote ile kusaini makubaliano yoyote kinyume na misingi ya katiba. Kwa msingi huo, Mfalme Salman wa Saudi Arabia na Al Sisi wanapasa kufuta makuabalino hayo ya kuchora upya mipaka ya nchi hizo.

Kiujumla tunaweza kusema kuwa ziara ya Mfalme wa Saudi Arabia huko Misri na propaganda nyingi zilizopigwa na pande mbili hizo kuhusu safari hiyo na vile vile kufikiwa makubaliano kati ya nchi mbili katika ziara hiyo, khususan suala la kuipatia Saudia visiwa viwili vilivyotajwa, inatathminiwa kuwa ni aina fulani ya kudhoofisha nafasi ya kieneo ya Misri na serikali ya al Sisi kukubali udhaifu huo.