Safari ya Bin Salman nchini Pakistan, mgeni aliyesusiwa na wenyeji
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51633-safari_ya_bin_salman_nchini_pakistan_mgeni_aliyesusiwa_na_wenyeji
Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman aliwasili jana Jumapili nchini Pakistan akiandamana na ndege saba na akisindikizwa na ndege kadhaa za kijeshi za Pakistan. Safari hiyo inafanyika chini ya ulinzi mkali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 18, 2019 07:29 UTC
  • Safari ya Bin Salman nchini Pakistan, mgeni aliyesusiwa na wenyeji

Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman aliwasili jana Jumapili nchini Pakistan akiandamana na ndege saba na akisindikizwa na ndege kadhaa za kijeshi za Pakistan. Safari hiyo inafanyika chini ya ulinzi mkali.

Kabla ya Bin Salman kuwasili mjini Islamabad, serikali ya Pakistan ilikata mawasiliano yote ya simu za mkononi na kusambaza maelfu ya askari katika barabara iliyotumiwa na mwanamfalme huyo hadi katika makao ya Waziri Mkuu ambako ndiko alikofikia. Vilevile Serikali ya Islamabad imeitangaza siku ya leo Jumatatu kuwa ni siku ya mapumziko ili kuzuia maandamanano ya wananchi wanaopinga safari ya Bin Salman nchini kwao. Zaidi ya wanajeshi elfu 12 wakiwemo walinzi binafsi wa Bin Salman wanalinda usalama mjini Islamabad. Licha ya kwamba serikali ya Pakistan imepamba mitaa na baadhi ya maeneo ya jiji la Islamabad kwa ajili ya Bin Salman lakini wananchi wa mji huyo wamesusia safari hiyo ambayo imecheleweshwa kwa siku moja kwa kuhofia maandamano ya wananchi.

Wapakistan wakiandamana kupinga safari ya Bin Salman

Wapakistan wanalalamikia sera za Saudi Arabia katika eneo la Mashariki ya Kati hususa vita na mashambulizi ya nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Yemen, njama za serikali ya Riyadh dhidi ya Syria na misaada na uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi na vilevile kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Isarel unaoendelea kuua raia wa Palestina bila ya huruma. Wananchi wa Pakistan pia wanaamini kuwa, sera za nchi za Kiarabu za kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo zimeisababishia Pakistan matatizo mengi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Kiarabu zinataka kuitumbukiza zaidi Pakistan katika migogoro ya kikanda kama vita vya Yemen kwa ajili ya kufikia malengo yao, suala ambalo limeitwisha Islamabad mzigo mkubwa wa kiuchumi na matatizo mengi ya kisiasa. 

Viongozi wa serikali ya Islamabad wanasema kuwa, Bin Salman anatazamiwa kutia saini mikataba kadhaa ya uwezekezaji unaokadiriwa kufikia dola bilioni 20 lakini wakosoaji wanasema gharama kubwa zilizotumiwa na serikali kwa ajili ya maandalizi na mapokezi hayo haziwezi kuhalalishwa katika mtazamo wa kiuchumi. Wachambuzi hao wanakosoa ubadhirifu mkubwa uliofanywa na serikali ya Imran Khan kwa ajili ya maandalizi ya ngeni kutoka nje ya nchi. Wanauliza, ziko wapi nara na kaulimbiu za Imran Khan za kubana matumizi ya fedha za umma? Katika uwanja huo gazeti la Ummat la Pakistan limeandika kuwa: "Mbali na Bin Salman, serikali ya Islamabad inagharamia watu elfu moja na mia moja wanaoandamana na mwanamfalme huyo wa Saudia pamoja na wahudumu wake na suala hili haliwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile."

Safari ya Bin Salman nchini Pakistan

Vilevile gazeti la Marekani la The Wall Street Journal limeandika kuwa: "Katika safari yake ya nchi kadhaa za Asia, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia anataka kupunguza hali ya kutengwa kimataifa na kuonesha kuwa ana ushawishi katika upeo wa kimataifa."

Safari ya sasa ya Bin Salman katika nchi kadhaa za Asia iliyoandamana na makelele mengi ya kipropaganda inakumbusha ile iliyofanywa na kiongozi huyo mwanagenzi katika nchi kadhaa za kaskazini mwa Afrika mwezi Novemba mwaka jana ambayo iliandamwa na maandamano makubwa ya wananchi na kulazimika kufupisha safari hiyo. Kwa msingi huo inatazamiwa kuwa, safari ya sasa ya Bin Salman pia haitakuwa na mwisho bora kuliko ile ya kabla yake. Mwanamfalme huyo anajaribu kusafisha sura chafu ya nchi yake Saudi Arabia na yeye mwenyewe baada ya mauaji ya kutisha ya mwandishi na mkosoaji wa serikali ya Riyadh, Jamal Khashoggi tena ndani ya ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki.

Bin Salman

Kwa kutilia maanani hayo yote wanachambuzi wengi wa mambo wanasema, safari hizo za Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia na udiplomaia wa kumwaga pesa na kutaka kununua watawala wa nchi mbalimbali kwa fedha za mafuta hakutaweza kusafisha sura chafu na mikono iliyojaa damu ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen, Iraq na Syria ya watawala wa Saudi Arabia.