Mar 08, 2019 13:46 UTC
  • Amnesty International yaitaka Saudia iwaachie huru wanaharakati wa kike

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitisha maandamano mbele ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Paris huko Ufaransa kulalamikia hatua ya serikali ya Riyadh ya kuendelea kuwashikilia wanaharakati wa kike wa kutetea haki za binadamu.

Maandamano hayo yamefanyika sambamba na maadhisho ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke kote duniani.

Amnesty International imesema kuwa, baadhi ya wanaharakati wa kike wanaoshikiliwa katika korokoro za Saudi Arabia wamefanyiwa ukatili na kuteswa kama ya kufungwa nyaya zenye umeme, kutandikwa mijeledi na kutishiwa kunajisiwa.

Washiriki katika maandamano hayo mbele ya ubalozi wa Saudia mjini Paris wamewataka madereva kupiga honi na ving’ora vya magari yao kama ishara ya kuonesha mshikamano wao na wanaharakati wa kike wanaoteseka katika korokoro za Saudia.

Maandamano ya leo mbele ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Paris yamefanyika siku moja tu baada ya nchi 36 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kutoa taarifa iliyolaani ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia na kutoa wito wa kuachiwa huru wanaharakati wa kike wanaoshikiliwa kwa sababu tu ya kutetea haki za wanawake na haki za binadamu kwa ujumla.

Wanaharakati wa kike wanasota jela Saudi Arabia

Ripoti za mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu zinasisitiza kuwa, wanaharakati wa kike wa kutetea haki za binadamu wanaoshikiliwa mahabusu tangu miezi kumi iliyopita huko Saudia wanasumbuliwa na ukandamizaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kuteswa na hata ukatili wa kingono ambavyo vinasimamiwa na Saud al Qahtani aliyekuwa mshauri wa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman.

Tags