Apr 16, 2019 14:43 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Hali ya kibinadamu nchini Yemen inasikitisha mno

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi mkubwa ulionao kutokana na kutoridhisha kabisa hali ya kibinadamu nchini Yemen

Hayo yameelezwa katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kujadili hali ya mambo nchini Yemen ambapo maafisa wa Umoja wa Mataifa wamelieleza baraza hilo kuhusu wasiwasi wao juu ya machafuko yanayozidi kuongezeka katika maeneo mengine ya Yemen na nje ya mji wa bandari wa al-Hudaydah ambako mkataba wa kusitisha mapigano unaendelea kutekelezwa.

Mark Lowcock ambaye ni Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, ameliambia Baraza la Usalama, “wakati usitishaji mapigano katika mji wa bandari wa al-Hudaydah unaendelea kuheshimiwa, tumeshuhudia kuongezeka kwa vurugu katika maeneo mengine ya nchi kama kule Hajjah, kaskazini mwa al-Huudaydah na katika mji wa Taiz.”

Hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen

Kuhusu hali ya kibinadamu, Bwan Lowcock ameonya kuwa, kuna uwezekano wa mlipuko wa kipindupindu ambapo tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2019, takribani visa 200,000 vya kipindupindu vimeripotiwa. Hiyo ni takribani mara tatu zaidi ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita yaani 2018. Takribani robo ya visa vyote ni watoto chini ya umri wa miaka mitano, amesema.

Saudi Arabia, ikishirikiana na waitifaki wake kadhaa wa eneo, ilianzisha vita dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuurejesha madarakani utawala kibaraka na tiifu kwa Riyadh.

Nchi kadhaa za Magharibi, hususan Marekani na Uingereza zinaupatia muungano huo vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia silaha na zana za kisasa za kijeshi pamoja na misaada ya kilojistiki na kiintelijensia.

Tags