Hamas: Hila ya Marekani ya kutaka kutekeleza "Muamala wa Karne" haitafanikiwa
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa hila ya serikali ya Marekani ya kutaka kutekeleza mpango kwa jina la Muamala wa Karne haitafanikiwa.
Hazem Qassim amesema kuwa mapambano dhidi ya maghasibu wanaoikalia kwa mabavu Palestina yataendelea hadi nchi huru ya Palestina itakapoundwa huku mji mkuu wake ukiwa Baitul Muqaddas. Msemaji wa Hamas ameyasema hayo katika radiamali yake kwa hatua ya kuwekwa wazi mikakati mipya kuhusu mpango huo wa Marekani na Wazayuni wa Muamala wa Karne. Wakati huo huo Yuval Steinitz Waziri wa Nishati wa utawala wa Kizayuni amekaribisha maelezo mapya yaliyowekwa wazi katika mpango huo wa Muamala wa Karne.
Jared Kushner mkwe na mshauri wa Rais Donald Trump wa Marekani jana alieleza kuwa marhala ya kwanza ya mpango wa Muamala wa Karne inalenga kuwekeza dola bilioni 50 huko katika ardhi za Palestina, Misri, Jordan na Lebanon.
Mpango huo uliopendekezwa na Marekani kwa jina la "Muamala wa Karne" unajumuisha kuiunganisha kikamilifu Quds Tukufu na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, kuviunganisha vitongoji vilivyopo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na utawala huo, kufuta kikamilifu haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi za mababu zao na kuainisha eneo la Abu Dis kama mji mkuu wa nchi ya Palestina. Mpango huo umekabiliwa na radiamali kali ya Waislamu na wananchi wa Palestina; huku ukizidisha ghasia na mapigano kati ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni na Wapalestina khususan katika Ukanda wa Ghaza.