Imarati yaondoa idadi kubwa ya askari wake kutoka Yemen
Umoja wa Falme za Kiarabu umewaondosha nchini Yemen idadi kubwa ya wanajeshi wake.
Duru za kidiplomasia za nchi za Magharibi zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, Imarati iliwaondoa karibuni hivi wanajeshi wake nchini Yemen baada ya kushtadi taharuki baina ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili la Asia Magharibi.
Wanadiplomasia wanne wamenukuliwa na Reuters wakisema kuwa, UAE imelazimika kupunguza idadi ya wanajeshi wake baada ya kuongezeka wasiwasi wa kutokea vita katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Taharuki hiyo ilishtadi baada ya Marekani kuongeza idadi ya wanajeshi na zana zake za kivita zikiwemo manowari za kijeshi katika eneo hili. Washington ilichukua hatua hiyo ikidai kuwa inajiandaa kukabiliana na kile ilichokitaja kuwa tishio la Iran.
Hata hivyo baadhi ya duru za habari zimedokeza kuwa, Abu Dhabi imechukua uamuzi huo baada ya kushuhudia wimbi la vipigo kutoka kwa vikosi vya Yemen vikisihirikiana na kamati za wananchi.
Saudia kwa kushirikiana na Imarati, Marekani, Israel, na nchi nyingine za Ulaya na Kiarabu ilianzisha mashambulizi makali dhidi ya Yemen kuanzis mwezi Machi 2015, sambamba na kuizingira kila upande nchi hiyo.
Hadi sasa vita hivyo vimepelekea zaidi ya watu elfu 16 kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa. Wengi wa wahanga wa hujuma hizo ni raia wa kawaida wasio na hatia na hasa wanawake na watoto wadogo.