Wasaudia waendelea kulalamikia kualikwa mwanamuziki mcheza uchi nchini mwao
Wanaharakati wengi wa mitandao ya kijamii na wananchi wa Saudi Arabia wamekasirishwa mno na kualikwa mwanamuziki mmoja wa RAP wa Kimarekani katika tamasha la muziki la mjini Jeddah.
Tamasha la muziki la Jeddah linatarajiwa kufanyika tarehe 17 Julai mwaka huu chini ya usimamizi wa Taasisi ya Burudani na Starehe ya Saudi Arabia ambapo mwanamuziki wa Kimarekani, Nicky Minaj anatarajiwa kutumbuiza.
Wanaharakati wa mitandano ya kijamii wa Saudi Arabia wamelalamikia vikali tamasha hilo na kusema kuwa, litamkaribisha mwanamuziki wa Kimarekani anayecheza uchi jukwaani na kupinga vikali siasa za mabadiliko za mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohamed bin Salman.
Baada ya kutangazwa na baba yake kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Bin Salman amekuwa akifanya kila njia kujionesha kuwa ni mpenda mageuzi na amekuwa akichukua hatua mbalimbali za kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na siasa za kigeni za Saudi Arabia.
Mabadiliko yake ya kijamii yanaiga vigezo vya madola ya Magharibi visivyo vya Kiislamu na visivyo vya kimaadili, jambo ambalo linalalamikiwa vikali na Waislamu kote ulimwenguni.
Uvamizi wa Yemen na kuendelea kuwaua kwa umati wananchi Waislamu wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu, mauaji dhidi ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi na masheikh na wanazuoni mbalimbali akiwemo Ayatullah Nimr Baqir Nimr, kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini Saudi Arabia ni sehemu ndogo ya jinai nyingi zilizofanywa na Bin Salman hasa baada ya kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia.