Saudia yakasirishwa na Imarati kupunguza askari wake Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54714-saudia_yakasirishwa_na_imarati_kupunguza_askari_wake_yemen
Watawala wa Saudi Arabia wameghadhabishwa mno na kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu cha kuwaondosha nchini Yemen idadi kubwa ya wanajeshi wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 12, 2019 10:44 UTC
  • Maiti za askari wa Imarati waliouawa Yemen
    Maiti za askari wa Imarati waliouawa Yemen

Watawala wa Saudi Arabia wameghadhabishwa mno na kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu cha kuwaondosha nchini Yemen idadi kubwa ya wanajeshi wake.

Hayo yameripotiwa na gazeti la New York Times la Marekani ambalo limenukuu duru kadhaa za kidiplomasia zikizungumzia hatua hiyo ya Imarati. Vyanzo hivyo vya habari vimeliambia gazeti hilo kuwa, kitendo hicho cha Imarati hakijawakasirisha tu watawala wa Aal-Saud, bali pia kimetoa pigo kubwa kwa madola ya Magharibi.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, UAE imechukua hatua ya kupunguza idadi kubwa ya askari wake kutokana na kulemewa na gharama kubwa ya vita dhidi ya Wayemen, na ndiposa imeamua kuchukua hatua hiyo bila kujali iwapo itaghadhabisha muitifaki wake, Saudia.

Wanadiplomasia wanne wamenukuliwa na shirika la habari la Reuters wakisema kuwa, Imarati imelazimika kupunguza idadi ya wanajeshi wake baada ya kuongezeka wasiwasi wa kutokea vita katika eneo la Ghuba ya Uajemi. 

Askari wa Imarati wakibeba maiti za wenzao waliouawa Yemen

Hata hivyo baadhi ya duru za habari zimedokeza kuwa, Abu Dhabi imechukua uamuzi huo baada ya kushuhudia wimbi la vipigo kutoka kwa vikosi vya jeshi la Yemen vikisihirikiana na kamati za wananchi.

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Umoja wa Falme za Kiarabu umeripotiwa kupunguza karibu asilimia 80 ya wanajeshi wake kutoka mji wa bandari wa al-Hudaydah huko kusini mwa Yemen.