Ansarullah yashambulia maeneo muhimu ya kijeshi mjini Riyadh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55613-ansarullah_yashambulia_maeneo_muhimu_ya_kijeshi_mjini_riyadh
Msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ametangaza kuwa, wapiganaji wa harakati hiyo wamefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya kituo muhimu sana cha kijeshi katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 26, 2019 08:50 UTC
  • Ansarullah yashambulia maeneo muhimu ya kijeshi mjini Riyadh

Msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ametangaza kuwa, wapiganaji wa harakati hiyo wamefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya kituo muhimu sana cha kijeshi katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.

Mashambulizi hayo ya leo yamefanyika siku moja tu baada ya harakati hiyo ya Ansarullah kushambulia maeneo kadhaa ya Saudia kwa makombora ya balestiki.

Yahya Saree amesema kuwa, kikosi cha ndege zisizo na rubani cha Ansarullah kimefanya mashambulizi makubwa dhidi ya eneo muhimu la kijeshi mjini Riyadh kwa kutumia ndege kadhaa zisizo na rubani aina ya Samad-3.

Amesema kuwa mashambulizi hayo ni jibu dhidi ya jinai na uhalifu unaoendelea kufanywa na muungano wa Saudia dhidi ya taifa la Yemen na amewataka raia wa Saudia kuwa mbali na vituo na kambi za kijeshi ambazo amesema ni shabaha halali za wanamapambano wa Yemen.

Katika kipindi cha msaa 24 yaliyopita harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kuwa imefanya hujuma kubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya balestiki dhidi ya kambi ya jeshi la anga ya Mfalme Khalid, maegesho ya ndege za kivita na jengo la mawasiliano, na vilevile dhidi ya uwanja wa ndege wa Abha huko Saudi Arabia.

Makombora ya Ansarullah Yemen yameua makumi ya askari wa Saudia

Yahya Saree amesema mashambulizi ya makombora ya Badr-1 dhidi ya uwanja wa ndege wa Jizan nchini Saudia yameua makumi ya watu. Amesisitiza kuwa mashambulizi hayo ndiyo makubwa zaidi ya makombora ya balestiki na ya masafa ya kati ya harakati ya Ansarullah tangu Saudi Arabia na washirika wake waivamie Yemen mwezi Machi mwaka 2015.