Shambulio la Saudia laua familia nzima akiwemo mama mjamzito Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60177-shambulio_la_saudia_laua_familia_nzima_akiwemo_mama_mjamzito_yemen
Saudi Arabia imetekeleza shambulizi la roketi katika mkoa wa Sa'ada, kaskazini magharibi mwa Yemen na kuua watu wote wa familia moja.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Apr 05, 2020 03:26 UTC
  • Shambulio la Saudia laua familia nzima akiwemo mama mjamzito Yemen

Saudi Arabia imetekeleza shambulizi la roketi katika mkoa wa Sa'ada, kaskazini magharibi mwa Yemen na kuua watu wote wa familia moja.

Kanali ya televisheni ya al-Masira imeripoti kuwa, baba, mkewe mjamzito na watoto wao wawili wameuawa katika shambulizi hilo la kikatili baada ya nyumba yao kulengwa na roketi la Saudia katika eneo la BeniSayyah, wilaya ya Razih mkoani Sa'ada.

Mkoa wa Sa'ada, kaskazini magharibi mwa Yemen mpakani mwa Saudia umekuwa ukishambuliwa karibu kila siku na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh, ambapo mbali na raia kuuawa, lakini pia miundimsingi ya mkoa huo imeharibiwa vibaya na hujuma hizo za anga.

Jana vyombo vya habari vya Yemen viliripoti kuwa, muungano huo vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen umetekeleza mashambulio 19 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Vikosi vamizi vinavyoongozwa na Saudia vinaishambulia Yemen tokea 2015

Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya al-Masirah, maeneo yaliyoandamwa na mashambulio ya vikosi vamizi vinavyoongozwa na Saudi Arabia ni Sa'adah, Ma'rib, Imran na Hajjah.

Hivi karibuni kituo cha Haki za Binaadamu cha Ain Al-Insaniyah kilielezea kuuawa na kujeruhiwa zaidi ya Wayemen elfu 42 katika kipindi cha miaka sita ya uvamizi na mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia nchini Yemen.