Onyo la Taliban dhidi ya kutoheshimu Marekani makubaliano ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60352-onyo_la_taliban_dhidi_ya_kutoheshimu_marekani_makubaliano_ya_amani
Kundi la wanamgambo wa Taliban limeonya kuwa, kutoheshimu Marekani hati ya makubaliano ya amani ya Doha Qatar kutakuwa sababu ya kuendelea vita nchini Afghanistan na kwamba, Washington ndio itakayobeba dhima ya hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 13, 2020 21:58 UTC
  • Onyo la Taliban dhidi ya kutoheshimu Marekani makubaliano ya amani

Kundi la wanamgambo wa Taliban limeonya kuwa, kutoheshimu Marekani hati ya makubaliano ya amani ya Doha Qatar kutakuwa sababu ya kuendelea vita nchini Afghanistan na kwamba, Washington ndio itakayobeba dhima ya hilo.

Taarifa ya Taliban imeeleza kuwa, kuendelea mashambulio ya mabomu na kukiuka wanajeshi wa Marekani makubaliano ya amani ya Qatar, ni hatua zilizo dhidi ya amani ambazo zinatoa pigo kwa mwenendo wa amani uliokuwa umeanza nchini humo. Wanamgambo wa Taliban wametangaza kuwa, mazungumzo ya amani baina ya kundi hilo na makundi mengine ya Afghanistan yataanza baada ya kuachiliwa huru wanachama wake kutoka katika magereza ya serikali.

Taarifa yenye onyo ya wanamgambo wa Taliban dhidi ya Marekani kuhusiana na kukiuka Washington makubaliano ya amani baina ya pande mbili yaliyotiwa saini Februari 29 huko Doha mji mkuu wa Qatar, ni ishara ya wazi kwamba, mazungumzo ya hivi karibuni baina ya wawakilishi wa pande mbili hizo hayakuwa na mafanikio yoyote.

Moja ya duru za mazungumzo ya Marekani na Taliban yaliyokuwa yakifanyika huko Doha Qatar

Baada ya serikali ya Kabul kubadilisha siasa zake kuhusiana na suala la kuwaachilia huru wanachama wa Taliban wanaoshikiliwa katika magereza ya nchi hiyo, iliamuliwa kuwa, wafungwa 1,500 wa Taliban waachiliwe huru. Taliban sambamba na kupinga mwenendo huo iliitaka Marekani itekeleze ahadi yake iliyotoa ya kuachiliwa huru wafungwa wote wa kundi hilo kabla ya kuanza mazungumzo baina ya Waafghani.

Kuweko udiriki na ufahamu tofauti kuhusiana na makubaliano ya amani ya Doha baina ya Marekani na wanamgambo wa Taliban na kila upande kuutuhumu upande wa pili kwamba, umekuwa ukikiuka vipengee vya makubaliano hayo, kulitoa msukumo wa kufanyika mkutano baina ya wawakilishi wa pande mbili hizo huko nchini Afghanistan ili kufanya mazungumzo kuhusiana na namna ya kutekeleza makubaliano hayo.

Katika mazingira ya sasa, kuachiliwa huru wanachama wote wa Taliban wanaoshikiliwa katika magereza ya Afghanistan  unatathminiwa kama mtihani wa kuipima Marekani ni kwa namna gani inaheshimu na kufungamana na ahadi zake na kwamba, kwa mujibu wa wanamgambo hao kutekelezwa kikamilifu kwa makubaliano hayo ni sharti la lazima la kufanyika mazungumzo baina ya Waafghani.

Wanamgambo wa Taliban

Filihali, kundi la wanamgambo wa Taliban limejikita zaidi juu ya suala la kuachiliwa huru wanachama wake walioko jela ambapo kidhahiri inaonekana kuwa, haiwezekani kutegemea mashinikizo ya Marekani dhidi ya serikali ya Kabul kwa ajili ya kufikia lengo hilo.

Kuibuka mgogoro nchini Marekani kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona kumekuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Rais Donald Trump. Hali hii imeifanya serikali ya Trump takribani isitishe ufuatiliaji wa mafaili muhimu katika uga wa siasaza kigeni na badala yake kutumia nguvu zake zote kwa ajili ya kujinasua kutoka katika kinamasi cha janga la virusi vya Corona.

Nchini Afghanistan nako, kuendelea mpasuko wa kisiasa na vita vya madaraka baina ya Abdallah Abdallah na Muhammad Ashraf Ghani nako kwa namna fulani kumeibua hali ya mparaganyiko katika ufuatiliaji wa masula ya ndani ya nchi hiyo.

Abdallah Abdallah na Ashraf Ghani mahasimu wawili wa kisiasa nchini Afghanistan

Ni kwa kuzingatia mazingira hayo ambapo baada ya kutokuwa na natija mazungumzo ya wawakilishi wa Taliban na Marekani yaliyofanyika huko nchini Afghanistan kwa ajili ya kujadili namna ya kutekeleza makubaliano ya amani ya Qatar, wanamgambo hao wametoa taarifa yenye indhari kuhusiana na kukiuka mara kwa mara Washington hati ya makubaliano hayo ya amani, ambapo sehemu ya onyo hilo imeashiria mashambulio mtawalia ya wanajeshi wa Marekani katika maeneo mbalimbali ya Afghanistan.

Hata hivyo kundi la Taliban limeashiria kuendelea mashambulio ya Marekani nchini Afghanistan kama ukiukaji wa mara kwa mara wa Washington kwa makubaliano ya amani, katika hali ambayo, kundi hilo nalo liliendeleza mashambulio yake katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo siku moja tu baada ya kutia saini makubaliano hayo ya amani. Kutotekeleza Taliban ahadi yake ya kupunguza vitendo vya utumiaji mabavu nchini Afghanistan, mbali na kuibua malalamiko nchini humo, kumekuwa sababu ya serikali ya Kabul kubadilisha mwenendo wake wa namna ya kuwaachilia huru wafungwa wa kundi hilo.