Saudi Arabia katika kinamasi cha Yemen
Hali ya sasa ya Yemen inaonyesha kuwa, viongozi wa Saudi Arabia wamepatwa na kiwewe na kukosa la kufanya kuhusiana na yanayojiri katika nchi hiyo jirani.
Kuna dalili nyingi za kiwewe hicho cha watawala wa ukoo wa Aal Saud kuhusiana na hali ya Yemen. Kuchanganyikiwa huko kwa upande mmoja kunaonekana katika mienendo ya Riyadh kuhusiana na Serikali ya Uokovu wa Kitaifa inayondwa na harakati ya Ansarullah na washirika wake, na katika upande mwingine kuhusiana na yanayojiri ndani ya muungano wa kusini mwa Yemen na hujuma ya Saudi Arabia na waitifaki wake dhidi ya taifa la nchi hiyo.
Ushahidi unaonyesha kuwa, Saudia imefikia natija kwamba, uwezo wa kijeshi wa jeshi la Yemen na harakati ya wananchi ya Ansarullah umeongezeka kwa kiasi kikubwa cha kuweza kusababisha madhara na hasara isiyofidika kwa utawala wa Riyadh. Vipigo mtawalia kama kile cha mwaka 2019 dhidi ya vituo vikubwa zaidi vya mafuta vya Saudi Arabia katika miji la Abqaiq na Khurais, ambavyo vilipelekea kupungua nusu ya uzalishaji wa mafuta wa nchi hiyo viliweka alama ya kuuliza kuhusiana na uwezo wa kijeshi na kisiasa wa serikali ya Riyadh. Kwa msingi huo Saudia ilianza kutafuta njia ya kujiondoa katika kinamasi cha Yemen na imekubali mapendekezo ya kusitisha vita ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo suala la kuondoka Yemen mikono mitupu peke yake linahesabiwa kuwa ni kipigo kingine na fedheha kubwa, na sambamba na kukubali pendekezo la kusitisha vita, utawala huo unaendelea kushambulia maeneo mbalimbali ya Yemen.
Kuhusiana na suala hilo, mkuu wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Uokovu Yemen yenye makao yake katika mji mkuu wa nchi hiyo, San'aa Muhammad Abdusalam ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba: "Usitishaji vita wa upande mmoja haujatekelezwa na kinyume chake, muungano vamizi umezidisha hujuma na mashambulizi yake ya anga."
Wakati huo huo yanayojiri ndani ya muungano huo vamizi pia yanaakisi picha ya kuchanganyikiwa na kukosa mwelekeo Saudi Arabia. Hitilafu kubwa baina ya Riyadh na Abu Dhabi ndani ya muungano huo kuhusiana na eneo la kusini mwa Yemen zilianza mwaka jana baada ya Imarati kutangaza kuwa, inawaondoa wanajeshi wake nchini Yemen. Novemba mwaka jana na kupitia makubaliano ya Riyadh, Saudia ilifanya jitihada za kupunguza hitilafu hizo; hata hivyo ushahii unaonyesha kuwa, kinyume chake, migawanyiko na hitilafu zimepamba moto zaidi na sasa lile linalojiita Baraza la Mpito la kusini mwa Yemen linalodhibitiwa na Imarati linaendeleaza mikakati ya kudhibiti maeneo makubwa na kujiimarisha zaidi kusini mwa Yemen.
Katika mkondo huo huo duru za Yemen zimeripoti kuwa, kikosi kamili cha wapiganaji wa liyekuwa rais wa Yemen aliyekimbikia Saudia, Abdrabbuh Mansur Hadi kimejiunga na wanamgambo wa Baraza la Mpito linalodhibitiwa na Imarati katika kisiwa cha Socotra.
Harakati hizi ni kielelezo cha kuimarika zaidi kundi la wanaotaka kujitenga eneo la kusini mwa Yemen na kushadidi mvutano na hitilafu baina ya Saudi Arabia na Imarati. Mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, As’ad Bishara anasema: Kunashuhudiwa migongano ya Saudia na Imarati huko kusini mwa Yemen na jitihada za kuzidisha satua na ushawishi wa kila mmoja wao, na matokeo ya mivutano hiyo ni hali inayoonekana katika maeneo ya Al Mahrah na Socotra.
Vita dhidi ya taifa la Yemen pia ni miongoni mwa sababu kuu za nakisi kubwa ya bajeti ya Saudia na kuongezeka kwa asilimia 130 ya gharama za kijeshi za nchi hiyo tangu mwaka 2015 hadi mwaka jana wa 2019. Aal Saud wameelewa kwamba, ili kuzuia mwenendo huo wa kuongezeka nakisi ya bajeti kuna udharura wa kusitisha gharama za masuala ya kijeshi. Hata hivyo kupenda jaha na ukubwa kwa mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman kwa upande mmoja, na kushindwa kutimiza hata lengo moja kati ya malengo ya kuanzisha vita huko Yemen, kunaifanya Saudia ichanganyikiwe na kushindwa la kufanya baina ya kusitisha vita au kuendeleza hujuma na mashambuizi dhidi ya taifa hilo.
Nukta ya mwisho ya kuashiria katika uchambuzi huu ni kwamba, kadiri Aal Saudi wanavyozidi kuchanganyikiwa kuhusiana na vita vya Yemen, ndivyo kadiri jeshi na makundi ya kujitolea ya wananchi wa Yemen yanavyoimarika na kupata nguvu kubwa zaidi za kukabiliana na wavamizi hao.