Maafa ya kibinadamu Yemen yafika kileleni kutokana na sera za Marekani
Baada ya Marekani kukata mchango wake kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), shirika hilo limetangaza kukata asilimia 80 ya misaada yake kwa watu wa Yemen.
Matukio ya sasa ya Yemen yanaweza kuangaziwa kwa mitazamo miwili. Mtazamo wa kwanza ni wa wanajeshi wa Jeshi la Yemen na wapiganaji wa kamati za kujitolea za wananchi ambao wameweza kupata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya Saudia na hivi sasa wana uwezo wa makombora na wa ndege zisizo na rubani unaomtisha adui. Katika upande wa pili kuna mzingiro wa pande zote wa Yemen ambao unatekelezwa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na hivyo kufanya hali ya kibinadamu kuwa mbaya sana nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni, watu milioni 22 kati ya watu wote milioni 24 nchini Yemen wanahitaji msaada wa kibinadamu. Taarifa ya Shirika la Afya Duniani inaonyesha kuwa hivi sasa watoto 15,000 nchini Yemen wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa lishe. Aidha takribani Wayemen milioni 15 hawapati huduma za tiba na afya baada ya kufungwa vituo va afya nchini humo.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kutoa Misaada la OXFAM, tokea Januari 2017 hadi Disemba 2019, takriban watoto milioni 2 na laki mbili nchini Yemen waliambukizwa kipindupindu.
Yusuf al-Hadhri, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Yemen ametangaza mwezi huu wa Aprili kuwa, katika mwaka huu wa 2020, Wayemen 80,000 wameambukizwa kipindupindu.
Mbali na hayo, watu wa Yemen wanaugua pia magonjwa mengine mengi kama vile Malaria na Homa ya Dengue.
Katika hali kama hii, Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye nchi yake sasa inakabiliwa na janga kubwa la corona ameonyesha udhaifu mkubwa wa utendaji katika kukabiliana na janga hilo na ili kufunuika kufeli kwake, sasa analaumu Shrika la Afya Duniani (WHO) kuwa eti ndilo linalohusika katika kuenea corona. Kwa msingi wa madai hayo, Trump amekata mchango wa nchi yake wa dola milioni 400 kwa WHO.
Lise Grande Mratibu Mkaazi wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Yemen katika radiamali yake kufuatia sera hiyo mpya ya Marekani amesema WHO imekata asilimia 80 ya bajeti yake ambayo ilikuwa ikitoa kwa hospitali na huduma za dharura katika sekta ya afya nchini humo.
Ripoti zinaonyesha kuwa kukatwa misaada ya WHO kutakuwa na athari mbaya sana kwa utendaji na pengine hata kupelekea kufungwa hospitali 189 na vituo 200 vya kiafya nchini Yemen.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, sekta ya afya ya Yemen ni kati ya sekta ambazo zilimeathirika vibaya zaidi kutokana na hujuma shadidi za ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia ambao unapata uungaji mkono kamili wa Marekani. Muungano huo wa Saudia umekuwa ukidondosha mabomu kiholela kaika mahosptali na vituo vya afya na hivyo kusababisha hasara kubwa.
Wizara ya Afya ya Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa ya Yemen inasema ili kuweza kufanikiwa katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 au corona inahitaji vifaa 500,000 vya kupima corona katika awamu ya kwanza na vifaa milioni 10 katika awamu ya pili.
Katika kukabiliana na corona, Yemen inakumbana na matatizo makubwa kama vile uhaba wa mashine za kusaidia wagonjwa kupumua, vitanda vya vitengo vya ICU na mitungi ya oxigeni. Sambamba na hali hiyo ya kusikitisha Saudi Arabia imekiuka madai yake ya usitishaji vita Yemen na inaendelea kudodonsha mabomu katika nchi hiyo masikini zaidi Asia Magharibi.
Hakuna shaka kuwa, Yemen kukatiwa misaada ya WHO, ambayo ni taasisi muhimu zaidi ya misaada ya kiafya, na kisha kuendelea uvamizi wa Saudia dhidi ya nchi hiyo ni mambo ambayo yatafanya hali ya kibinadmau ya Wayemen kuzidi kuwa mbaya katika wakati huu ambapo nchi hiyo tayari imetajwa kuwa yenye maafa mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.