Aliyekuwa mchumba wa Khashoggi asikitishwa na Saudia kuruhusiwa kununua New Castle
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60904-aliyekuwa_mchumba_wa_khashoggi_asikitishwa_na_saudia_kuruhusiwa_kununua_new_castle
Mchumba wa Jamal Khashoggi, mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud aliyeuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki mwaka 2018 ameeleza kusikitishwa kwake na mpango wa kuuruhusu utawala wa Aal-Saud ukiongozwa na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman ununue asilimia 80 ya hisa za klabu ya soka ya New Castle ya Uingereza kwa thamani ya dola milioni 300.
(last modified 2026-08-14T10:24:44+00:00 )
May 10, 2020 19:52 UTC
  • Aliyekuwa mchumba wa Khashoggi asikitishwa na Saudia kuruhusiwa kununua New Castle

Mchumba wa Jamal Khashoggi, mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud aliyeuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki mwaka 2018 ameeleza kusikitishwa kwake na mpango wa kuuruhusu utawala wa Aal-Saud ukiongozwa na mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman ununue asilimia 80 ya hisa za klabu ya soka ya New Castle ya Uingereza kwa thamani ya dola milioni 300.

Katika mahojiano na BBC ya Uingereza jana Jumapili, Khadija Genghis ameitaka klabu hiyo pamoja na Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza (EPL) kutoa kipaumbele kwa thamani za utu badala ya thamani za kifedha.

Khadija Genghis amesema "tunapaswa kuzingatia thamani za kimaadili, si thamani za kifedha na kisiasa tu. Pesa haziwezi kununua kila kitu katika dunia hii, huu ndio ujumbe muhimu unaopaswa kuwafikia watu kama Mrithi wa Ufalme (wa Saudia). Wale wanaohusishwa na mauaji na ukatili hawapaswi kupewa nafasi yoyote katika soka la Uingereza."

Mchumba huyo wa Khashoggi anaomba wote waliohusika na ukatili huo washtakiwe na kuadhibiwa, kuanzia wale wa ngazi za juu kabisa hadi wa chini kabisa akisisitiza kwamba, itakuwa ni fedheha kubwa iwapo EPL itaidhinisha muamala huo.

Bin Salman (kulia) na Khashoggi

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa Agnès Callamard amewahi kutangaza kwamba, kumepatikana nyaraka na ushahidi madhubuti unaothibitisha kwamba maafisa wa ngazi za juu wa Saudi Arabia akiwemo Muhammad bin Salman walihusika na mauaji ya mwandishi na mkosoaji mkubwa wa utawala wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi. 

Tarehe pili Oktoba mwaka 2018, maafisa 15 wa serikali ya Saudi Arabia walitumwa mjini Istanbul Uturuki wakitokea Riyadh kwenda kumuua mwandishi huyo wa habari aliyekuwa anaukosoa utawala wa hivi sasa wa Riyadh.

Serikali ya Saudi Arabia awali ilikanusha kuhusika na mauaji hayo, lakini baada ya mashinikizo kuwa makubwa ililazimika kukiri kuwa timu ya mauaji iliyomuua kinyama Jamal Khashoggi ilitumwa na serikali kwenda kumsaili mwandishi huyo na kwamba eti aliuawa kimakosa katika usaili huo.