Ziara ya Pompeo katika ardhi za Palestina na malengo yake kadhaa
Uhusiano wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel umepanuka sana kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika wakati huu wa urais wa Donald Trump huko Marekani ambaye amechukua hatua nyingi za kutekeleza kivitendo matakwa haramu ya 'Israel.'
Licha ya kuenea ugonjwa wa corona na Marekani kufuta takriban safari zote za viongozi wa nchi hiyo nje ya nchi, lakini Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Jumatano asubuhi alifanya safari ya siku moja katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la 'Israel' akiwa na malengo kadhaa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imedai kuwa, lengo la ziara hiyo ni mambo matatu. Mosi ni sehemu ya juhudi za pande mbili za kupambana na ugonjwa wa COVID-19. Pili ni kwa ajili ya kutathmini harakati za Iran katika eneo hili, na tatu ni kuhusu uamuzi wa upande mmoja wa utawala wa Kizayuni wa kuliteka eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kwamba, ijapokuwa hayo yanaweza kuwa sehemu ya malengo ya safari hiyo, lakini kuna malengo mengine ambayo huenda ni muhimu zaidi kwa Trump ambayo hayakutangazwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Miongoni mwa malengo hayo muhimu ni hamu kubwa ya Trump ya kupata uungaji mkono wa Wazayuni katika kampeni zake za uchaguzi. Hivi sasa Trump amepoteza sana uungaji mkono wa ndani ya Marekani kutokana na uzembe alioufanya katika vita dhidi ya corona. Hivyo kinachotarajiwa katika ziara ya hivi sasa ya Mike Pompeo huko 'Israel' ni kumuona waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani anatangaza kuunga mkono misimamo yote ya utawala wa Kizayuni. Kabla ya kuondoka Marekani, Pompeo alisema katika mahojiano aliyofanyiwa kwamba, hatari ya Iran na kuizuia Tehran eti isimiliki silaha za nyuklia, ndiyo ajenda kuu za safari yake huko 'Israel.'

Ikumbukwe kuwa, muda wote utawala wa Kizayuni unaitaka Marekani iongeze vikwazo dhidi ya Iran na jambo hilo limekuwa likisemwa hadharani mara kwa mara na viongozi wa utawala huo pandikizi hasa waziri mkuu wake, Benjamin Netanyahu ambaye daima anadai kuwa eti Iran inafanya harakati za siri za kumiliki silaha za nyuklia. Katika upande mwingine, serikali ya Donald Trump huko Marekani nayo iliamua kutekeleza kivitendo siasa za Wazayuni za kuiwekea Iran vikwazo ambavyo Washington inajigamba kuwa ni vya kiwango cha juu kabisa ambavyo haijawahi kuwekewa nchi nyingine yoyote ghairi ya Iran. Ndoto za Trump na Wazayuni wenzake ni kuona shughuli zote za nyuklia za Iran zinasimama. Si hayo tu, lakini pia Wazayuni hao wana ndoto ya kuona miradi ya makombora na shughuli za kiulinzi za Iran zote zinasimama, na misimamo Tehran nayo inabadilika kikamilifu na kufuata ile ya Wazayuni.
Pompeo amesema, Trump amefanya mambo mawili kwa namna ya kipekee, moja na kuiwekea vikwazo vikubwa Iran na pili ni kwamba atahakikisha Iran haimiliki 'silaha' za nyuklia.
Hata hivyo matamshi hayo ya Pompeo ni kichekesho kikubwa. Kwanza viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba, kama walikuwa na nia kweli ya kumiliki silaha za nyuklia, basi hakuna dola lolote lingeliweza kulizuia taifa la Iran kumiliki silaha hizo. Lakini kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukukfu ya Kiislamu, kumiliki silaha za maangamizi ya umati zikiwemo za nyuklia ni haramu, hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina haja kabisa na silaha za nyuklia. Pili Trump na kundi lake wameshindwa kutimiza hata lengo lao moja la kuiwekea "mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi" Iran. Kwani shughuli za amani za nyuklia za Iran ya Kiislamu zinaendelea kama kawaida, shughuli za kiuchumi zinaendelea, misimamo ya Iran imezidi kuwa imara, kamwe Iran haitokwenda kuipigia magoti Marekani na mambo mengineyo mengi.

Amma kuhusiana na uamuzi wa kutekwa ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuunganishwa na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na Wazyuni, Nabil Abu Rudeineh, msemaji wa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema, madai ya balozi wa Marekani, David D. Friedman kwamba uamuzi wa kutekwa ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuingizwa chini ya utawala wa Kizayuni ni uamuzi wa Israel, si kweli hata kidogo, kwani hiyo ni sehemu ya mpango wa 'Muamala wa Karne' uliopendekezwa na Marekani na ni katika njama za Washington za kuiangamiza kikamilifu nchi ya Palestina.
Kiujumla ni kwamba, Trump hivi sasa anahitajia mno uungaji mkono wa Wazayuni katika kampeni zake za uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba 2020 huko Marekani. Hivyo kusitarajiwe chochote cha kheri katika ziara ya Mike Pompeo huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.