Aug 25, 2020 03:30 UTC
  • HAMAS yaionya Israel kuhusiana na kushadidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeuonya utawala haramu wa Israel kuhusiana na kushadidisha mashambulio na mzingiro wake dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS  amesema kuwa, kuendelea uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza pamoja na mzingiro wake, ni uvamizi mtawalia dhidi ya taifa la Palestina ambao utawala wa Kizayuni unapaswa kubeba dhima ya matokeo yake mabaya.

Fawzi Barhoum amesema bayana kwamba, kushadidi mzingiro dhidi ya Gaza na hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuzuia kupelekwa katika eneo hilo bidhaa muhimu kama nishati na dawa, ni hatua ambayo katu haitateteresha azma na irada thabiti ya Palestina ya kusimama kidete dhidi ya madhalimu na wavamizi.

Eneo la Gaza linakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS  amezitaka asasi za kisheria na jamii ya kimataifa kufanya kila ziwezalo kuhitimisha uvamizi na mzingioro wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Aidha ameitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina kutekeleza ipasavyo majukumu yake mkabala na wananchi wanaokabiliwa na mzingiro wa Gaza.

Eneo la Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya miaka 14 sasa limekuwa chini ya mzingiro wa anga, baharini na nchi kavu unaotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel. Mzingiro huo umeyafanya maisha ya wakazi wa eneo hilo kuwa mabaya na hata kukabiliwa na maaafa ya kibinadamu kutokana na kukosa mahitaji muhimu ya maisha kama chakula na dawa.

Tags