Netanyahu: Tunafanya mazungumzo ya siri na nchi nyingi za Kiarabu
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema Tel Aviv hivi sasa inafanya mazungumzo ya siri na viongozi wengine wengi wa nchi za Kiarabu, juu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi hizo.
Benjamin Netanyahu amesema makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kidiplomasia baina ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu yamezifungulia mlango nchi nyingine za Kiarabu wa kuazisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu.
Kauli ya Netanyahu imekuja katika hali ambayo, hii leo na kwa mara ya kwanza, ndege ya utawala pandikizi wa Israel ya El-Al inatazamiwa kupita katika anga ya Saudi Arabia kabla ya kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Abu Dhabi nchini Imarati.
Riyadh ilikubali hapo jana ombi la Tel Aviv la ndege yake aina ya LY971 kutumia anga ya Saudia kwa mara kwanza, katika kile kinachoonekana ni wimbi la nchi za Kiarabu la kuanza kudhihirisha mahusiano yao na Israel.

Ndege hiyo ya utawala wa Kizayuni imebeba wajumbe wa Israel na wapambe wa karibu wa Rais Donald Trump wa Marekani akiwemo mshauri wake, Jared Kushner.
UAE na utawala wa Kizayuni tarehe 13 mwezi huu zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati yao. Mapatano hayo yaliyofikiwa kufuatia mashinikizo ya Marekani yamelaaniwa vikali katika kona mbalimbali za dunia.