Watunisia waandamana kuonyesha uungaji mkono wao kwa Wapalestina
Kwa mara nyingine tena wananchi na shakhsia mbalimbali wa Tunisia wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Tunis, kutangaza uungaji mkono wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina.
Shirika la habari la IRIB limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, wananchi hao wa Tunisia walioshiriki maandamano hayo kadhalika wamelaani hatua ya baadhi ya tawala za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waandamanaji hao wametangaza mshikamano wao na wananchi wa Palestina na kusisitiza kwamba, lengo la mapatano hayo ni kuwapotosha walimwengu kuhusu kadhia ya Palestina.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais wa Tunisia, Kais Saied kutoa mwito kwa walimwengu kushirikiana kuhakikisha kuwa Wapalestina wanakombolewa kutoka kwenye makucha ya utawala wa Kizayuni na wanapata haki zao.
Septemba 15, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na utawala wa kiimla wa Bahrain zilisaini makubaliaono ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ikulu ya White House nchini Marekani, na kusaliti malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.
Njama za tawala za kidikteta za Kiarabu za kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni zinafanyika katika hali ambayo, kwa miaka mingi Wazayuni wanawakandamiza Wapalestina na wanafanya jinai za kila anuai katika maeneo mbalimbali ya Kiarabu na Kiislamu.