Jan 29, 2021 02:07 UTC
  • UN yabainisha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka mapigano huko al Hudaydah, Yemen

Umoja wa Mataifa umesema kuwa, una wasiwasi kutokana na kuongezeka mapigano kati ya wapiganaji wa harakati ya Ansarullah na wale wa serikali iliyojiuzulu ya Yemen katika eneo la kistratejia la al Hudaydah.

Umoja wa Mataifa jana Alhamisi ulitoa taarifa na kaushiria raia wa Yemen waliopoteza maisha kwenye mapigano hayo na pia makazi na mashamba ya watu yaliyoharibiwa katika mapigano huko kusini mwa bandari ya al Hudaydah na kueleza kuwa: mapigano yaliyoanza katika eneo hilo kuanzia kati kati ya mwezi Januari mwaka huu yamepelekea kuwa wakimbizi familia 100 sawa na watu wasiopungua 700. 

Eneo hilo linahesabiwa kuwa sehemu muhimu ya kupokelea bidhaa za chakula na misaada mbalimbali ya kibinadamu kutoka nje. Umoja wa Mataifa umetahadharisha katika taarifa yake hiyo kuhusu mashambulizi ya kiholela katika maeneo ya makazi ya raia na kuyataja kuwa yanakiuka haki za binadamu. Umesema kuwa, mashambulizi hayo yanapaswa kusitishwa mara moja. 

Maafa ya mapigano katika mji wa bandari wa al Hudaydah 

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la Ufaransa ilizopata tarehe 18 mwezi Januari mwaka huu kupitia duru za kijeshi na kitiba; katika muda wa wiki moja ya mapigano karibu wanachama 150 wa Ansarullah na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali iliyojiuzulu huko Yemen na pia raia wanane ambao aghalabu yao ni wanawake na watoto waliuawa katika eneo hilo. 

Wakati huo huo wakazi wa mji wa bandari wa al Hudaydah wameeleza kuwa, hayo ni mapigano makali zaidi kushuhudiwa katika eneo hilo tangu kuanza kutekelezwa usitishaji vita mwezi Disemba mwaka 2018  chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. 

Tags