Yemen: Umoja wa Mataifa utekeleze jukumu lake la kulinda raia
Msemaji wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa ya Yemen amesema: "Umoja wa Mataifa unapaswa kuchukua hatua ya kuzishinikiza nchi ambazo zimeivamia Yemen ili ziliende maisha ya raia."
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Masira, Daktari Najib Al-Qabati, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Uwokozi wa Kitaifa ya Yemen jana Jumatatu aliashiria hujuma ya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya nyumba ya makazi katika eneo la al-Hok mkoani Al Hudayda ambapo raia watano wa familia moja waliuawa na kusema: "Kushambuliwa makazi ya raia ni ishara kuwa muungano vamizi unaongozwa na Saudia unalenga raia kwa makusudi jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu." Amesema jinai za Saudia na mamluki wake zinafanyika huku jamii ya kimataifa ikiwa imenyamaza kimya.
Daktari al-Qabati aidha amesema muungano vamizi wa Saudia unazuia mafuta ya petroli kuingia Yemen jambo ambalo limepelekea kusitishwa huduma za kitiba katika baadhi ya hospitali na zahanati nchini Yemen.
Wizara ya Afya ya Yemen pia hivi karibuni ilitangaza kuwa muungano vamizi wa Saudia umeizingira nchi hiyo na kuzuia vifaa vya kitiba kuwafikia watu wa Yemen na hivyo kupelekea sekta ya afya nchini humo kukumbwa na matatizo makubwa.
Ikumbukwe kuwa kuanzia Machi 2015, Saudi Arabia kwa uungaji mkono wa Marekani, Umoja wa Falme za Kiarbau na nchi kadhaa zingine ilianzisha hujuma ya kijeshi dhidi ya Yemen na kuizingira nchi hiyo angani, nchi kavu na baharini.
Ndege za kivita za Saudia na watifaki wake hadi sasa zinaendeleza mashambulizi dhidi ya Yemen ambapo makumi ya maelfu ya raia, hasa wanawake na watoto wameuawa na mamilioni ya Wayemen wamelazimika kuwa wakimbizi.