Iraq yasisitiza kufanyika mazungumzo ya kitaifa na ushirikiano wa kieneo
Waziri Mkuu wa Iraq amewasilisha miito na mpango kwa ajili ya mazungumzo ya kitaifa na kushirikiana nchi za eneo ili kuimarisha amani na maelewano.
Akizungumza jana Jumatatu mwishoni mwa safari ya kihistoria ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis huko Iraq, Mustafa al Kadhimi amesistiza kuwa safari hiyo ni nukta adhimu na ya kung'ara katika historia ya nchi hiyo ambayo imeonyesha dhati ya taifa la Iraq kwa walimwengu. Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa ujumbe wa Papa na timu aliyoongozana nayo huko Iraq umefikisha matakwa ya wananchi wa Iraq kwa walimwengu.
Al Kadhimi ameongeza kuwa, tangu ilipoundwa serikali ya Iraq imekuwa ikifuatilia suala la kuhuisha na kurekebisha mahusiano yake ya nje na nchi hiyo na juhudi zimekuwa zikifanywa ili kurejesha nafasi ya kawaida ya Iraq katika eneo na ulimwenguni kwa ujumla.
Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Khadhimi aidha ameyataka makundi yote ya kisiasa, wanaharakati wa makundi ya kiraia, vijana wanaoandamana na wapinzani wa serikali waketi kwenye meza ya mazungumzo, watangulize kwanza maslahi ya kitaifa na kujiepusha na mazungumzo yenye kuibua mivutano. Amesema serikali inapasa kupatiwa fursa ya kutosha ili kuandaa na kuendesha uchaguzi kwa mujibu wa misingi imara.
Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Ijumaa iliyopita aliwasili Baghdad mji mkuu wa Iraq katika safari yake ya kwanza baada ya kupita karibu miezi 15 ya kuenea maambukizi ya corona duniani na kupelekea kuakhirishwa safari yake hiyo.