Hujuma ya kigaidi yaua watu 8 katika hujuma Herat, Afghanistan
Watu wasiopungua wanane wameuawa na wengine 47 kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi mkoani Herat magharibi mwa Afghanistan.
Gavana wa Herat Sayed Abdul Wahid Qatali amesema wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouawa katika hujuma hiyo iliyotekelezwa usiku wa kuamkia Jumamosi kwa kutumia bomu la kutegwa ndani ya gari.
Kwa mujibu wa Msemaji wa hosptitali ya mkoa huo, Mohammad Rafiq Sherzai, idadi ya vifo baada ya mlipuko huo ulioharibu nyumba 14 inatarajiwa kuongezeka kwa sababu majeruhi wengi wako katika hali mbaya.
Msemaji wa Wazira ya Mambo ya ndani Tariq Arian amesema, mmoja kati ya waliouawa na 11 waliojeruhiwa ni wafanyakazi wa vikosi vya usalama, huku wengine wakiwa ni raia, miongoni mwao wanawake na watoto.
Katika taarifa, Umoja wa Mataifa umelaani ongezeko la mashambulizi yanayolenga raia nchini Afghanistan licha ya juhudi za mazungumzo ya amani kati ya serikali na kundi la Taliban. Hakuna kundi lolote lililojitokeza kudai kuhusika na shambulizi hilo.
Hayo yanajiri wakati ambao, Wizara ya Mambo ya Nje ya Afghanistan imetangaza kuwa ujumbe unaoiwakilisha serikali ya nchi hiyo utashiriki katika kikao cha amani kuhusu Afghanistan kilichopangwa kufanyika huko Moscow mji mkuu wa Russia.
Kikao kuhusu amani ya Afghanistan kinatazamiwa kufanyika Alhamisi ijayo Machi 18 huko Moscow mji mkuu wa Russia.
Hatua ya serikali ya Afghanistan ya kutangaza utayarifu wake wa kushiriki kikao cha amani chini ya uwenyeji wa Russia huko Moscow mji mkuu wa nchi hiyo baada ya kugonga mwamba mazungumzo kati ya makundi ya Kiafghani huko Doha mji mkuu wa Qatar, inatathminiwa kuwa yenye kuleta matumaini mapya kwa serikali na wananchi wa Afghanistan ili kuhitimisha vita na kurejesha amani na utulivu nchini humo.