Yemen: Marekani inapaswa kuchukua hatua kivitendo ili kuhitimisha vita
Mjumbe mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema, Marekani inapaswa kuchukua hatua kivitendo ili kuhitimisha vita dhidi ya nchi hiyo.
Muhammad Ali al Houthi ameayasema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa twitter kujibu matamshi aliyotoa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken aliyedai kuwa, Washington inaongeza juhudi za kidiplomasia kwa ajili ya kuhitimisha vita nchini Yemen.
Muhammad Ali al Houthi ameeleza, "aliyonena Blinken kuhusu kusitishwa uingiliaji wa kigeni nchini Yemen ni matamshi chanya, lakini tunachongojea sisi ni hatua ya kivitendo ya Washington kuhusu kujiondoa askari wa jeshi la Marekani na washauri wao katika vita vya Yemen."
Mjumbe huyo mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesisitiza: "Sisi tunasubiri tangazo la kukiamuru kikosi cha majini cha jeshi la Marekani kiondoe mzingiro dhidi ya Yemen."
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price ametangaza kuwa, wakati waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Antony Blinken alipokutana hivi karibuni na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen Martin Griffith, alisema, Washington inataka, kwa ushirikiano Umoja wa Mataifa na pande zinginezo, kuzidisha juhudi za kidiplomasia kwa ajili ya kukomesha vita vya Yemen.
Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani.
Moto wa vita uliowashwa na Saudia na washirika wake dhidi ya Yemen umeshasababisha maelfu ya Wayemeni kuuawa, makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kupoteza makazi yao na kuwa wakimbizi.../