Saudi Arabia; mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha ulimwenguni
Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stokholm (SIPRI) imetangaza kuwa, kuanzia mwaka 2016 hadi 2020 Saudi Arabia iliongeza kwa asilimia 61 ununuzi wa silaha ikilinganishwa na kipindi cha kati ya 2011 na 2015.
Ripoti ya taasisi ya SIPRI kuhusiana na Saudia tunaweza kuigawa katika sehemu mbili.
Sehemu ya kwanza ya ripoti hiyo inahusiana na kuongezeka kwa kiwango kikubwa cha kununuliwa na kutumwa silaha katika eneo la Asia Magharibi baina ya mwaka 2016 hadi 2020. Ripoti hiyo inaeleza kuwa, zaidi ya thuluthi moja ya silaha zilizonunuliwa duniani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita zilinunuliwa kutoka Marekani na nusu ya silaha hizo zilitumwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Sehemu ya pili ya ripoti hiyo inahusiana na Marekani ambayo imetajwa kuwa muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani katika kipindi cha kati ya 2016 na 2020. Takribani nusu ya silaha zilizotengenezwa Marekani ambayo ni sawa na asilimia 47 zilizouzwa na kupelekwa katika eneo la Asia Magharibi zilinunuliwa na saudia Arabia.
Aidha asimilia 76 ya silaha zilizonuliwa na Saudia zilitoka Marekani. Hili ni jambo ambalo kabla ya kitu chochote libainisha utambulisho wa uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia.
Fauka ya hayo, sehemu ya tatu ni kadhia ya Saudia ya kuzingatia masuala ya kijeshi ambayo haijaashiriwa katika ripoti hiyo ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stokholm (SIPRI). Gharama za kijeshi za Saudia kuanzia 2016 hadi 2020 zilikuwa zaidi ya dola bilioni 273 na gharama hizi ni asilimia 20.9 ya gharama zote za utawala wa nchi hiyo.
Kwa kuzingatia takwimu hizi inawezekana kusema kuwa, gharama za kijeshi zinaunda sehemu muhimu ya gharama za utawala wa Aal Saud. Hivi sasa swali linalojitokeza ni hili kwamba, kwa nini Saudi Arabia ndio nchi inayotenga bajeti kubwa zaidi ya matumizi ya kijeshi miongoni mwa nchi zilizoko katika mkondo wa kuendelea?
Sababu ya kwanza ya hilo ni kwamba, Saudia imeingia katika vita dhidi ya Yemen. Katika uwanja huo, duru za habari zimetangaza kuwa uchunguzi kuhusiana na takwimu za bajeti ya Saudia unaonyesha kuwa, kwa kuzingatia nchi hiyo kujiingiza katika vita vya Yemen, matumizi ya kijeshi katika bajeti ya Saudia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kimekuwa kikubwa kuliko matumizi katika sekta ya elimu na afya.
Kwa maneno mengine ni kuwa, vita dhidi ya Yemen vimekuwa sababu ya kuongezeka gharama na matumizi ya kijeshi ya utawala wa Aal Saud.
Viongozi wa Aal Saud wanaamini kwamba, kuzuia kutokea mabadiliko ya mlingano wa nguvu katika eneo la Asia Magharibi kunaweza kufanyika kupitia vita na uingiliaji wa masuala ya ndani ya mataifa mengine. Hii ni katika hali ambayo, vita ni chimbuko kuu la kuongezeka gharama za nchi hiyo na vilevile kutokea nakisi ya bajeti sambamba na matatizo ya kiuchumi yanayowakabili hivi sasa wananchi wa Saudi Arabia.
Sababu ya pili ni kuwa, utawala wa kifamilia wa Aal Saud unaona kuwa, kubakia kwake kuna mfungamno, utegemezi pamoja na himaya kutoka nje. Utegemezi huu ni mkubwa kiasi kwamba, mashinikizo kutoka nje dhidi ya Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufame wa Saudia katika faili la mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi yamehatarisha juhudi zake za kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo na kumrithi ufalme baba yake.
Kwa kuzingatia utegemezi huu utawala wa Aal Saud hauna budi ghairi ya kutumia sehemu kubwa ya pato lake kwa ajili ya kununua silaha kutoka kwa madola makubwa ya Magharibi. Rais aliyepita wa Marekani Donald Trump mara kadhaa aliidhalilisha Saudia na kutangaza wazi kwamba, kama Washington itasitisha himaya na uungaji mkono wake kwa Riyadh basi utawala huo utakabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama.
Kiwango kikubwa cha Saudia kununua silaha kutoka Marekani kabla ya kila kitu kinaweka bayana gharama inazotumia nchi hiyo ya Kiarabu kwa ajili ya kununua usalama kutoka kwa dola hilo la Magharibi. Silaha hizo zinanunuliwa katika hali ambayo, Saudia haikabiliwi na tishio lolote lile kutoka nje, bali siasa za chokochoko na kupenda makuu za nchi hiyo ndizo chanzo cha vitisho dhidi yake.
Nukta ya mwisho ni hii kwamba, katika hali ambayo, katika kipindi cha baina 2016 na 2020 kiwango cha Saudi Arabia kununua silaha kiliongezeka kwa asilimia 61 ikilinganishwa na miaka 2011 hadi 2015, mshirika muhimu wa nchi hiyo katika vita dhidi ya Yemen yaani Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), kiwango chake cha kununua silaha kilipungua kwa asilimia 37.